News
MAMIA YA WAJASIRIAMALI WANUFAIKA NA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KUTOKA NSSF
*Waamua kujiunga na kujiwekea akiba ili wanufaike na mafao
Na MWANDISHI WETU,
Dar es Saalam. Dhamira ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali ya wananchi imezidi kupamba moto baada ya mamia ya wajasiriamali katika masoko ya Ilala Boma, Mchikichini na Buguruni jijini Dar es Salaam, kuhamasika kujiunga na kuchangia NSSF ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko.
NSSF kupitia kwa Meneja wa Sekta isiyo rasmi, Bi. Rehema Chuma imeweka kambi kwenye masoko hayo kwa lengo la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya na kuhamasisha uchangiaji ambapo hamasa ya wajasiriamali kupata elimu na kujiunga imekuwa kubwa.
Baadhi ya wajasiriamali akiwemo Ally Omar, amesema amepata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kujiunga, kuchangia na kujiwekea akiba katika Mfuko na namna watakavyonufaika na mafao yanayotolewa.
Naye, Neema Swali, mjasiriamali katika soko la Ilala, amesema baada ya kupatiwa elimu ameamua kujiunga ili aweze kujiwekea akiba kwani ameona kuna faida nyingi anazonufaika nazo ikiwemo kupata pensheni ya uzeeni, fao la uzazi na matibabu.
NSSF imeweka utaratibu nzuri wa wajasiriamali kujiunga na kuchangia ambapo mwanachama baada ya kujiandikisha anapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na anapaswa kuchangia kuanzia shilingi 30,000 au 52,200 au zaidi kwa mwezi na anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi, muhula au msimu ili aweze kunufaika na mafao yote yanayotolewa ikiwemo ya uzee, urithi, uzazi, matibabu na msaada wa mazishi.