emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

MAMIA YA WASTAAFU WAJITOKEZA KUSIKILIZWA NA KUTATULIWA KERO ZAO NA WAZIRI NDALICHAKO


*Akutana na zaidi ya wastaafu 1000, wenyewe waridhishwa na utaratibu unaotumika kuwasikiliza

Na MWANDISHI WETU

Mamia ya wastaafu Mkoani Dar es Salaam wajitokeza kwa wingi katika mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako wa kuwasikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wastaafu.

Waziri Profesa Ndalichako leo tarehe 22 Julai, 2022 alikutana na baadhi ya wastaafu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa kukutana na wastaafu kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua changamoto zao mbalimbali ambapo mkutano huo ulianza juzi Mkoani Dodoma.

"Tayari kama mnavyoona kazi imeanza tunawasikiliza na tunatatua changamoto na kama nilivyosema Wizara yangu pamoja na mambo mengine ina dhamana ya kusimamia wastaafu wanaolipwa mafao kupitia Mfuko wa NSSF na PSSSF," alisema.

Waziri Ndalichako alisema hayo leo wakati alipokutana na wastaafu zaidi ya 1, 000 wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao wanahudumiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSSSF.

Aidha alisema anatambua kuwa wapo wastaafu ambao wanalipwa mafao yao kupitia Hazina kuwa wakifika katika mkutano huo kuna fomu watapewa kwa ajili ya kuzijaza na baadaye fomu hizo zitawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango.

"Tunao uwezo wa kutatua changamoto moja kwa moja za wastaafu ambao wanalipwa kupitia Mfuko wa NSSF na PSSSF," alisema.

Waziri Profesa Ndalichako alisema anathamini mchango mkubwa uliotolewa na wazee katika ujenzi wa Taifa hivyo atahakikisha kwa kushirikiana na watendaji wa NSSF na PSSSF changamoto zao zinasikilizwa, kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Alisema miongoni mwa changamoto za wastaafu aliokutana nao ni pamoja na mapunjo ya mafao na huku akisisitiza kuwa changamoto zote zitapatiwa ufumbuzi na kila mstaafu atapata huduma anayostahiki.