News
NPF ESWATINI WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO YA MFUMO WA MABADILIKO KUTOKA MFUMO WA AKIBA KWA WASTAAFU KWENDA MFUMO WA PENSHENI
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Mfuko wa Taifa wa Akiba (NPF), Eswatini walipofika kupata mafunzo na uzoefu kuhusu mfumo wa mabadiliko kutoka Mfuko wa Taifa wa Akiba (NPF) kwenda Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mabadiliko hayo yaliiwezesha iliyokuwa Mfuko wa Akiba wa Wafanyakazi (NPF) ulioanzishwa mwaka 1964 kubadilishwa na kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), mwezi Julai 1998.
Ziara hiyo iliongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NPF ya nchini Eswatini, Bi. Futhi Tembe pamoja na Meneja Mkuu Uendeshaji NPF, Bw. Miccah Nkabinde.
Katika kikao hicho, Meneja Usimamizi Mafao wa NSSF, Bw. James Oigo alitoa wasilisho namna mfumo wa mabadiliko ulivyofanyika kutoka NPF hadi kuwa NSSF. Alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuwa na Mfuko unaolipa mafao ya pensheni ya kila mwezi badala ya mafao ya akiba yaliyokuwa yanalipwa kwa mkupuo.
NSSF imeendelea kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki, na kuwa kivutio kikubwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi za SADC kwa ujumla kuja kujifunza na kujenga uzoefu wa namna ya kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuendesha sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kwa manufaa ya wanachama na wananchi.
Ziara hiyo ya mafunzo ya mfumo wa mabadiliko ilihudhuriwa pia na Menejimenti ya NSSF na ilifanyika wiki hii katika Ofisi za Makao Makuu ya NSSF, jijini Dar es Salaam.