emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YAENDELEZA KASI UTOAJI ELIMU YA HIFADHI YA JAMII MWANZA



Yaitaka jamii kutambua kuwa NSSF ni rafiki wa maisha yao ya sasa na ya baadaye

Wajasiriamali katika Mwalo wa Magomeni Kirumba Mwanza wachangamkia fursa wajiunga na kujiwekea akiba

Na MWANDISHI WETU,

Mwanza. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kufungua fursa kwa wajasiriamali na wavuvi wa Mwalo wa soko la Magomeni, jijini Mwanza ambao wamepatiwa elimu ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kujiwekea akiba kwa kujiunga na NSSF kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Akizungumza tarehe 17 Mei 2024 wakati akitoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali na wavuvi wa Mwalo huo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya amewataka wajasiriamali na wavuvi wa soko hilo kuchangamkia fursa ya elimu ya hifadhi ya jamii waliyopatiwa kwa kujiunga na kujiwekea akiba kwani NSSF ni rafiki wa maisha hivyo wasikubali kuishi bila ya rafiki huyo kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Bw. Mziya ametoa elimu hiyo ikiwa ni kuelekea kilele cha Malkia wa Nguvu, Kanda ya Ziwa ambapo Mfuko ni moja ya wadau kupitia kampeni ya ‘WEKA TUWEKE’ ya Clouds Media yenye fursa kwa makundi mbalimbali ambayo ni wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, wavuvi, wakulima, mama lishe, wafugaji na wajasiriamali wengine wote.

“Mtu anapopatwa na majanga mbalimbali rafiki mwema wa maisha yake ya sasa na ya baadaye ni NSSF, hivyo napenda kutoa wito kwa wajasiriamali, wavuvi, wakulima, mama lishe, wafugaji kuchangamkia fursa hii kwa kujiunga na NSSF ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko likiwemo la matibabu na pensheni ya uzee,” amesema Bw. Mziya

Amesema taratibu za kujiunga na NSSF ni rahisi sana na kujiandikisha ni bure ambapo baada ya mwanachama kujaza fomu yake atapatiwa kitambulisho chenye namba ya uanachama na hapo hapo ataweza kujichangia kila mwezi shilingi 30,000 ambayo itamuwezesha kunufaika na mafao yote yanayotolewa na

Mfuko.

“Lengo la NSSF ni kutoa pensheni lakini kuna maisha ya kujenga pensheni na maisha ya kula pensheni. Katika maisha ya kujenga pensheni unajiwekea kidogo kidogo na wakati unajenga pensheni unapata na mafao mengine kama matibabu na mafao ya uzazi kwa kina mama na kwa wale ambao watachangia mpaka kufikisha umri wa kustaafu watakuwa wanakula pensheni,” amesema Bw. Mziya.

Naye. Bi. Rehema Chuma, Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi ameendelea kutoa wito kwa wananchi waliopo kwenye makundi mbalimbali ya sekta isiyo rasmi kujiunga na kuchangia NSSF ili waweze kujenga kesho yao iliyokuwa njema. Amesema baadhi ya wanachama waliojiandikisha walipatiwa vitambulisho vyao hapo hapo.