News
NSSF YAHIMIZA MATUMIZI MIFUMO YA TEHAMA KWA WANACHAMA WAKE
Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewahimiza wanachama wake wakiwemo wastaafu watarajiwa kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kupata taarifa zao popote walipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NSSF, Bw. Robert Kadege wakati wa mafunzo ya siku tano kwa wastaafu watarajiwa Mkoa wa Dar es Salaam, yaliyoanza tarehe 1 Julai na kuhitimishwa tarehe 5 Julai 2024.
Katika mafunzo hayo NSSF ilikutana na wastaafu watarajiwa pamoja na baadhi ya waajiri kutoka Mkoa wa Temeke, Ubungo, Kinondoni, Kigamboni na Ilala na kuwaeleza umuhimu wa kufuatilia taarifa zao mbalimbali kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo inawawezesha waajiri na wanachama kupata taarifa zao popote walipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za Mfuko.
Bw. Kadege amesema NSSF imetengeneza PORTAL ambayo kwa upande wa waajiri (Employer Portal) inawarahisishia kuwasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati na vilevile kwa upande wa wanachama (Member Portal) wanaweza kufuatilia taarifa zao popote walipo bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
Naye, Meneja Malipo ya Pensheni wa NSSF, Bi. Nancy Mwangamila amewaeleza wastaafu watarajiwa umuhimu wa kuandaa taarifa zao za uanachama, kuhakiki majina na tarehe zao za kuzaliwa pamoja na taarifa za michango yao kama ipo sawa ili wakati wa kufungua madai ya kustaafu kusijitokeze changamoto yoyote kuhusiana na taarifa hizo.
Kwa upande wake, Meneja Mafao wa NSSF, Bw. James Oigo amesema kupitia mafunzo hayo wanawaondoa hofu wastaafu watarajiwa na kuwapa mbinu ya kuishi baada ya kustaafu ikiwemo kuwa na matumizi mazuri ya fedha, kufanya uwekezaji salama na kuepuka matapeli.
Awali, Bw. Mrisho Mwisimba, Meneja wa NSSF Mkoa wa Ilala, amewahakikishia wastaafu hao kuwa NSSF itaendelea kuwahudumia kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha muda wowote wanapohitaji usaidizi.