emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YAWAHAKIKISHIA WASTAAFU WATARAJIWA KUWA IKO IMARA NA INAENDELEA KULIPA MAFAO KWA WAKATI BILA USUMBUFU





*Yasema imejikita zaidi kutoa huduma kidijitali



Na MWANDISHI WETU,
Mbeya. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuwanoa wastaafu watarajiwa kwa kuwapa mafunzo ya kujiandaa kustaafu huku ukiwahakikishia kuwa utaendelea kulipa mafao yaliyoainishwa kwenye sheria kwa wakati bila ya usumbufu wowote.



Hayo yalisemwa na Bw. Robert Kadege, Meneja Huduma kwa Wateja wakati akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, amewahakikishia wastaafu wake kuwa NSSF iko imara na itaendelea kuwalipa wastaafu pensheni zao kila ifikapo tarehe 20 hadi 24 ya kila mwezi.



Bw. Kadege amesema hayo tarehe 22 Mei, 2024 jijini Mbeya ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo yaliyoandaliwa na NSSF kwa wastaafu watarajiwa wa mkoa huo ambao wamepatiwa elimu kuhusu namna bora ya kufanya maandalizi ya kustaafu, mafao mbalimbali yanayotolewa, fomula na jinsi ya kuendesha shughuli za kiuchumi ambazo wastaafu wanapaswa kuzifanya pamoja na elimu kuhusu afya.



“Naomba niwape salamu za Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba ambaye ameniambia niwahakikishie kuwa Mfuko wetu uko imara na endelevu na kuwa unaendelea kulipa mafao yaliyoainishwa kwenye sheria hivyo msiwe na wasiwasi wowote,” amesema Bw. Kadege.



Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Bw. Deus Jandwa amewashukuru washiriki wa semina hiyo kwa mwitikio mkubwa wa kuhudhuria mafunzo hayo ambapo amewahakikishia kuwa NSSF imejikita kutoa huduma zake kidijitali zaidi kupitia PORTAL ambayo kwa upande wa waajiri (Employer Portal) inawarahisishia kuwasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati na vilevile kwa upande wa wanachama (Member Portal) wanaweza kufuatilia taarifa zao popote walipo bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.



Aidha, Meneja Malipo ya Pensheni wa NSSF, Bi. Nancy Mwangamila amewaeleza wastaafu watarajiwa umuhimu wa kuandaa taarifa zao za uanachama, michango na kuwataka kwenda kuzihakiki kama zipo sawa ili wakati wa kufungua madai ya kustaafu kusijitokeze changamoto yoyote kuhusiana na taarifa hizo ili waweze kulipwa kwa wakati.



Meneja Huduma za Matibabu wa NSSF, Bi. Aisha Marine naye amesema huduma ya afya inatolewa kwa wanachama ambao wapo kwenye ajira na wanachangiwa michango yao kwa wakati bila kukosa pia kwa wastaafu wanaweza kupata huduma hiyo kwa kuchangia asilimia sita ya mafao ya pensheni ya kila mwezi kwa hiari yao kwa kuandika barua ya kuomba kukatwa asilimia hiyo ambayo itakatwa kwa muda wa miezi mitatu ndipo watakuwa wamefikia kigezo cha kupata huduma ya matibabu. Pia alitoa elimu ya namna bora ya kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.



Awali, Bi. Lydia Kimario, Afisa Mkuu Mafao ametoa mada kuhusu namna kukokotoa mafao na jinsi gani wanaweza kujiandaa kabla ya kustaafu.



Mzee Merthob Kapinga (76), amesema alistaafu utumishi mwaka 2008 na tokea kipindi hicho amekuwa akipokea pensheni yake kila inapofikia tarehe 22 ya kila mwezi. “NSSF inataka wanachama wake wasipate shida, nawashukuru sana kwani wanatusaidia na wanatujali wazee wastaafu,” amesema Mzee Kapinga.