News
NSSF YAWAJENGEA UWEZO WASTAAFU, YAWAHIMIZA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KUPATA TAARIFA ZAO MBALIMBALI
Na MWANDISHI WETU,
Mbeya. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendesha mafunzo kwa wastaafu watarajiwa zaidi ya 200 na kuwaeleza umuhimu wa kufuatilia taarifa zao mbalimbali kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo inawawezesha waajiri na wanachama kupata taarifa zao popote walipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
NSSF imetengeneza PORTAL ambayo kwa upande wa waajiri (Employer Portal) inawarahisishia kuwasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati na vilevile kwa upande wa wanachama (Member Portal) wanaweza kufuatilia taarifa zao popote walipo bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
Mafunzo hayo yamefunguliwa tarehe 21 Mei, 2024 jijini Mbeya na
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo, Bw. Emmanuel Kayuni, ambaye ameitaka NSSF kuendelea kutoa elimu hiyo hata kwa wafanyakazi wanaoanza kuajiriwa ili waweze kujipanga mapema na kustaafu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Bw. Robert Kadege amesema lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wastaafu watarajiwa ili waweze kuelewa mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali ambayo inarahisisha huduma kwa wanachama.
Bw. Kadege ametoa wito kwa waajiri wa sekta binafsi kulipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ( Employer Portal) ili kuwaondolea usumbufu wanachama pindi wanapostaafu kwa mujibu wa sheria.
Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Bw. Deus Jandwa amehimiza wafanyakazi kutumia mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha michango yao inawasilishwa kila mwezi kidijitali katika ofisi za NSSF
''Sasa hivi mifumo yetu imerahisishwa, unaweza ukaingia kwenye mifumo ya NSSF kwa kutumia simu yako ukaangalia michango kama mwajiri anakuletea au la na kama michango haiwasilishwi basi mfanyakazi anatakiwa kutoa taarifa NSSF ili tuchukue hatua kwa muhusika,'' amesema Bw. Jandwa.
Bi. Subira Lugala mmoja wa wastaafu watarajiwa ametoa wito kwa wafanyakazi ambao hawajajiunga na NSSF kujiunga ili waweze kustaafu kwa staha pindi wakati utakapofika.
Naye, Dkt. Maundi Keneth amesema semina hiyo imewatoa hofu na kujiandaa wanapoelekea kustaafu