News
WAZIRI SILAA AZUIA UTAPELI ENEO LA NSSF
*Ni baada ya NSSF kuweka mtego wa kuwakamata matapeli hao
*Walitaka ‘kumpiga’ Mama milioni nane, wakaishia mikononi mwa polisi
Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa amempa siku 14 Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha amewaondoa watu wote waliovamia ardhi inayomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mtaa wa Malela, Kata ya Toangoma Dar es Salaam.
Mhe. Silaa amesema hayo tarehe 5 Juni 2024 katika Mtaa wa Malela Toangoma mara baada ya kuwakamata watuhumiwa sugu wanne wanaodaiwa kuwatapeli wananchi na kuwauzia ardhi, baada ya NSSF kuweka mtego uliofanikisha kutiwa nguvuni kwa watuhumiwa hao.
Amesema kuanzia sasa anapiga marufuku Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kujihusisha na mauzo ya ardhi pamoja na nyaraka za Serikali za mitaa kutumika kuuzia viwanja na kuwa hivi sasa Wizara ya Ardhi inafanya marekebisho ya GN ya mwaka 2021, inayotoa nyaraka zinazotumika katika mauzo ya ardhi ambapo wanatarajia kutoa nyaraka mpya za kuuza maeneo nchini.
“Watu wa Serikali za Mitaa wakae mbali na shughuli za ardhi kwa hili watatusamehe nipo makini sana na masuala ya ardhi pamoja na utapeli wa ardhi unaoendelea,” amesema Mhe. Silaa.
Aidha, amewaagiza Polisi kuwakamata watuhumiwa hao ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria huku akimuagiza Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) kufanya operesheni maalumu katika eneo hilo ili kuwakamata watuhumiwa wengine na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Nataka niwapongeze wenzetu wa NSSF kwa kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hawa ambao wamekuwa wakifanya uhalifu wa kuuza maeneo ya NSSF na kuwadhulumu wananchi,” amesema Mhe. Silaa.
Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Malela, Oswin Mkinga amewashukuru NSSF kwa kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuwa maeneo hayo yanamilikiwa na NSSF na ni sehemu ya mradi wa viwanja 20,000 vya Toangoma ambavyo vilinunuliwa kwa utaratibu wa fidia mwaka 2000.
Amesema kuanzia mwaka 2000 mpaka 2023 utaratibu uliratibiwa na Wizara ya Ardhi kwa maana ya kuvipima na kuanza kuviuza, ambapo kuanzia mwaka 2019 alipoingia kwenye uongozi wa mtaa huo aliukuta uvamizi wa viwanja hivyo, lakini moja ya jitihada walizozifanya ni kutoa elimu kwa wananchi kuwa maeneo hayo ni mali ya NSSF na yanauzwa kwa utaratibu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja Miliki wa NSSF, Geofrey Timothy amemshukuru Mhe. Silaa kwa ushirikiano wake. Amesema walipewa taarifa kuwa eneo hilo kuna matapeli wanashiriki kuuza maeneo ya Mfuko na hivyo waliweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa matapeli hao.
“Ujumbe huu naomba ufike kwa wote waliovamia maeneo ya NSSF na pia ninawahakikishia wanachama wa NSSF kuwa maeneo yao yapo salama kwa sababu tuna utayari wa kutosha wa kuyafanya yawe salama,” amesema Timothy.
Mmoja ya waliotapeliwa kwa kuuziwa ardhi katika eneo hilo, Bi. Asha Ally Seif ameipongeza NSSF kwa kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwemo kumtafuta bibi na kudai hilo ni eneo lake jambo ambalo ni kinyume cha sheria.