News
NSSF kuwafikia waliojiajiri kupitia Hifadhi Skimu
*Vijana zaidi ya 1000 wa vyuo vikuu katika mkoa wa Morogoro wapata elimu ya hifadhi ya jamii
*Waziri Nanauka atambua mchango wa NSSF katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii
Na Mwandishi wetu.
Morogoro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Joel Nanauka, ameishukuru NSSF kwa mchango mkubwa katika kuifikia Sekta ya Hifadhi ya Jamii hususan kwa kufanikisha jukwaa la vijana lijulikanalo kama ‘Vijana Platform: campus Connect’ lililofanyika mwishoni mwa wiki katika chuo kikuu cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mheshimiwa Joel Nanauka amesema ushirikiano wa taasisi mbalimbali ikiwemo NSSF unaendelea kuwa chachu ya kusaidia shughuli mbalimbali zenye lengo la kuwasaidia vijana katika kupata maarifa, motisha na fursa mbalimbali za maendeleo. Ameeleza kuwa vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa hivyo wanahitaji kuandaliwa vizuri ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi.
Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu Watanzania milioni 25 ndio wenye uwezo wa kufanya kazi, na kati yao milioni 14 ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35. Hivyo, kusaidia shughuli zinazohusiana na vijana ni muhimu katika kuwawezesha kupata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kutimiza majukumu yao kwa ufanisi,” alisema Mheshimiwa Nanauka.
Aidha, alitambua jitihada zinazoendelea kufanywa na NSSF katika kusaidia maendeleo ya vijana nchini. Alieleza kuwa kupitia uwezeshaji wa NSSF, jukwaa hilo limefanikiwa kuwafikia vijana wengi mkoani Morogoro na hivyo kuwawezesha kupata maarifa kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo hifadhi ya jamii.
“Kupitia mchango wa NSSF tumeweza kufanikisha jukwaa hili la ‘Vijana Platform’ Morogoro na kuwafikia vijana wengi zaidi kwa kuwapatia maarifa yatakayowawezesha kuona na kutumia fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi,”
Alisisitiza kuwa jukwaa hilo litawasaidia vijana kupata maarifa yatakayowezesha kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
“Mafanikio hupatikana pale maandalizi yanapokutana na fursa. Jukwaa hili ni fursa muhimu kwenu vijana, hivyo litumieni vizuri kwa kusikiliza mada mbalimbali ili mfanye maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yenu,” alisema.
Aidha, aliwahakikishia vijana kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kwa kuwapatia taarifa, maarifa na fursa mbalimbali zitakazowasaidia kuendeleza mawazo na ubunifu wao.
Awali, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele, aliwahimiza wanafunzi kujenga utamaduni wa kuweka akiba hata kwa kiwango kidogo cha fedha wanachopata.
“Tunafahamu vijana wengi hawana kipato cha kudumu, lakini wanapata fedha kupitia mikopo ya elimu ya juu. Hivyo, kwa kujibana katika matumizi, wanaweza kuweka akiba hata ya shilingi 1,000 kwa siku ambayo itawasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema.
Bi. Mengele alieleza kuwa wanafunzi watakaojiunga na NSSF kupitia Hifadhi Skimu watanufaika na mafao mbalimbali, ikiwemo mafao ya matibabu ambayo yanasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi waliojiajiri hususan vijana.
“Ukiwa mwanachama wa NSSF utanufaika na mafao mengi, lakini leo nasisitiza mafao ya matibabu, ambayo yana umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa afya zenu,” alisema. Aidha, alisisitiza mfumo rafiki wa uchangiaji kupitia *152*00# unaweza mwananchi anaweza kujiunga na kuchangia huku akiendelea na shughuli za kiuchumi bila kulazimika kufika ofisi za NSSF.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Josephine Kapona, aliwataka vijana kulitumia jukwaa hilo kama mwanzo wa hatua mpya ya maendeleo yao.
“Ulizeni maswali, jengeni mitandao ya mawasiliano, tafuteni fursa na chukueni hatua,” alisema.

