emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YAHAWAKIKISHIA WASTAAFU KULIPWA MAFAO KWA WAKATI




Na MWANDISHI WETU,



Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewahakikishia wastaafu watarajiwa kuwa utaendelea kulipa mafao yaliyoainishwa kwenye sheria kwa wakati bila ya usumbufu wowote.



Hayo yalisemwa tarehe 2 Julai 2024 na Bw. Robert Kadege, Meneja Huduma kwa Wateja wa NSSF, ambapo alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa wanachama kufuatilia taarifa zao mbalimbali kupitia mifumo ya TEHAMA ambayo inawawezesha waajiri na wanachama kupata taarifa zao popote walipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.



Wastaafu hao watarajiwa walipatiwa mafunzo kuhusu namna bora ya kufanya maandalizi ya kustaafu, mafao mbalimbali yanayotolewa, fomula ya malipo ya mkupuo ya kustaafu na jinsi ya kuendesha shughuli za kiuchumi ambazo wastaafu wanapaswa kuzifanya.



Naye, Meneja Malipo ya Pensheni wa NSSF, Bi. Nancy Mwangamila amewaeleza wastaafu watarajiwa umuhimu wa kuandaa taarifa zao za uanachama, michango na kuwataka kwenda kuzihakiki kama zipo sawa ili wakati wa kufungua madai ya kustaafu kusijitokeze changamoto yoyote kuhusiana na taarifa hizo ili waweze kulipwa kwa wakati.



Kwa upande wake, Bw. Joseph Fungo, Meneja wa NSSF Ubungo ameeleza kuwa wanachama wana haki ya kufika katika ofisi za NSSF na kufuatilia taarifa zao kama ziko sahihi ambapo pia ameahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha.



Kwa upande wa wanachama wa NSSF, alikuwepo Athuman Mlinga ambaye ni mstaafu mtarajiwa ameishukuru NSSF kwa kuandaa semina hiyo ambayo imewawezesha kupata taarifa muhimu na kwa wakati sahihi kabla ya kustaafu.