News
NSSF YASHIRIKI SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI – MKOANI SINGIDA

Na Mwandishi Wetu, Singida
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, amewataka wafanyakazi wa Mfuko huo kuendelea kutoa huduma bora na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Mfuko unatimiza malengo uliyojiwekea.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wafanyakazi na wanamichezo wa NSSF walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Kitaifa (Mei Mosi), Bw. Mshomba alisema huduma bora kwa wanachama na wadau ndiyo msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma ikiwemo Mfuko wa NSSF.
“Tunao wajibu wa kuhakikisha kila mwanachama anahudumiwa kwa weledi na kwa wakati. Hili linawezekana tu endapo kila mmoja wetu atajituma zaidi na kuweka mbele maslahi ya Mfuko,” alisema Bw. Mshomba.
Hafla hiyo ilifanyika Aprili 30, 2025, mkoani Singida kuelekea siku ya Mei Mosi, ikiwa ni sehemu ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ndani ya Mfuko, katika michezo na ushiriki katika Wiki ya Usalama Mahala pa Kazi.
Alisema NSSF itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi na ari kwa wafanyakazi, lakini akasisitiza kuwa jitihada binafsi za kila mtumishi ndizo msingi wa mafanikio ya pamoja.
“Pamoja na juhudi tunazozifanya kuboresha mazingira ya kazi, tunahitaji kuona bidii na ubunifu zaidi kutoka kwenu – hasa katika eneo la ukusanyaji wa michango. Hili ni eneo muhimu linalobeba ustawi wa Mfuko,” aliongeza.
Katika hotuba hiyo, Bw. Mshomba alitoa pongezi kwa timu ya mpira wa kikapu ya NSSF kwa kushika nafasi ya tatu, na Bi. Agnetha Bimbiga aliyefanya vizuri katika mbio za riadha kwa kuwa mshindi wa pili katika mbio za mita 800 na 3,000 na kushika nafasi tatu katika mbio za mita 1,500.
“Haya ni mafanikio makubwa. Yameleta heshima kwa Mfuko na yanapaswa kuwa chachu ya kujituma zaidi hata katika maeneo ya kazi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa NSSF, Bw. Ekwabi Mujungu, alisema hafla hiyo ni sehemu ya kujenga mshikamano na kuimarisha utendaji wa watumishi na Mfuko kwa ujumla.
“Mafanikio tunayoyaona leo ni matokeo ya kazi ya pamoja na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi. Ni muhimu kuendeleza hali hii ili kufikia malengo ya Mfuko,” alisema Bw. Mujungu.
NSSF ilishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Bombadia, Singida, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani. Pia wafanyakazi wote wa NSSF walishiriki maadhimisho hayo katika kila mkoa Nchini.