News
NSSF yazidi kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali
.jpeg)
Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unaendelea na kasi ya utoaji elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi na wajasiriamali waliopo kwenye makundi mbalimbali, ambapo viongozi wa masoko ya Manzese na Mwananyamala, Dar es Salaam, kunufaika na elimu hiyo kwa ajili ya kujiunga na kujiwekea akiba ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko.
Akizungumza tarehe 14 Januari, 2025, Bw. Allen Mjindo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Manispaa ya Ubungo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina hiyo, amewahamasisha wajasiriamli wote wa manispaa hiyo kuchangamkia fursa ya kujiunga na kujiwekea akiba NSSF ili waweze kunufaika na mafao kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
“Niwapongeze NSSF kwa kuja na mpango huu wa kuifikia sekta isiyo rasmi, ni jukumu letu sisi viongozi kuwahamasisha wajasiriamali kujenga utamaduni wa kujiwekea kiba kwa kujiunga na kuchangia NSSF ili mwisho wa siku wanufaike na mafao mbalimbali yanayotolewa,” amesema Bw. Mjindo.
Naye, Bi. Rehema Chuma, Meneja wa Sekta isiyo rasmi, amesema katika muendelezo wa utoaji elimu ya hifadhi ya jamii, NSSF imeendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wa masoko ya Manzese na Mwananyama ili waweze kufikisha elimu hiyo kwa wajasiriamali wengine ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba.
“Lengo la mafunzo haya ni kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali kama vile wakulima, wavuvi, wafugaji, mama lishe, bodaboda, wachimbaji wadogo na wajasiriamali wengine wote ili wajiunge na mpango huu wa sekta isiyo rasmi na wanufaike na mafao ya uzeeni, urithi, uzazi na matibabu,” amesema Bi. Rehema.
Amesema lengo la kuanzishwa kwa Skimu ya Taifa ya Sekta isiyo rasmi ni kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na hifadhi ya jamii.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NSSF Ubungo, Bi. Gloria Gwanda, amesema Ofisi hiyo itahakikisha inawafikia wajasiriamali mbalimbali ili kuwaelimisha na kuwaandikisha kwa ajili ya kujiwekea akiba.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwahamasisha wajasiriamali hawa kujiunga na kujiwekea akiba NSSF ambayo itawasaidia katika maisha ya sasa na ya baadaye,” amesema Bi Gloria.
Meneja Mafao na Matibabu , Bi. Aisha Marine amesema NSSF inatoa mafao ya muda mrefu na muda mfupi yakiwemo ya matibabu ambapo mwanachama baada ya kujiunga anatakiwa kuchangia miezi mitatu mfululizo ili kunufaika na mafao hayo. Mwanachama akichangia shilingi 30,000 atapata matibabu yeye mwenyewe na akichangia shilingi 52,200 atanufaika yeye na wategemezi wake.
Aidha , Bi. Nuru Nhangachallo, mfanyabiashara wa soko la Mwananyamala, amepongeza NSSF kwa kuwapatia elimu ya hifadhi ya jamii ambayo itawasaidia kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema. Ameahidi elimu hiyo wataenda kuipeleka kwa wafanya biashara wenzao ili wajiunge na kujiwekea akiba.