News
Wastaafu Watarajiwa zaidi ya 1200 Waipongeza NSSF kwa Utoaji Semina ya Maandalizi ya Kustaafu
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
Wastaafu watarajiwa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam wameipongeza NSSF kwa kuandaa semina ya maandalizi ya kustaafu, wakieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa muhimu, mbinu bora na yatawasaidia namna bora ya kuishi pale ajira zao zitakapofikia mwisho baada ya kustaafu.
Semina hiyo ya siku tano imewafikia zaidi ya wastaafu watarajiwa 1200 kutoka makampuni mbalimbali jijini humo, ililenga kuwapatia washiriki uelewa wa kina kuhusu maandalizi ya kustaafu, ukokotoaji wa pensheni, mafao wanayostahili, elimu ya afya pamoja na elimu ya fedha iliyotolewa kwa kushirikiana na mabenki mbalimbali.
Awali akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa NSSF Mkoa wa Kigamboni, Bw. Siraji Kisaka, aliwahimiza wanachama wa NSSF kujenga tabia ya kuhakiki michango yao ya kila mwezi na kuwakumbusha waajiri wao pale wanapoona kuna ucheleweshaji wa uwasilishaji wa michango hiyo. Pia aliwasihi waajiri kuwasilisha michango kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Meneja wa Malipo ya Pensheni, Bi. Nancy Mwangamila, alisema Mfuko umeweka utaratibu mzuri wa matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kufungua na kufuatilia madai ya mafao, jambo linalorahisisha mchakato wa malipo na kuokoa muda.
Naye Bi. Floronce, ambaye ni mstaafu mtarajiwa, aliushukuru uongozi wa NSSF kwa kuandaa semina hiyo muhimu. Aidha, aliwataka wanachama wanaomaliza mikataba ya ajira kuendelea kuchangia kwenye mfuko huo wanapopata ajira au mikataba mipya ili waweze kunufaika na pensheni wanapostaafu.
Semina hiyo ya siku tano imehitimishwa leo katika Jengo la Mafao, Ilala, Dar es Salaam, ikiwahusisha wastaafu watarajiwa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam.

