emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​Huduma za NSSF zawafikia wananchi Kiwangwa



Na Mwandishi Wetu – Kiwangwa, Chalinze

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea na jitihada zake za kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi, safari hii ukifika katika eneo la Kiwangwa, Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani, maarufu kwa shughuli za kiuchumi zinazowahusisha wakulima, wavuvi na wajasiriamali wadogo.

Utoaji wa elimu hiyo ulifanyika hivi karibu, ukiongozwa na Meneja wa NSSF Mkoa wa Pwani, Bi. Witness Partick, ambaye alieleza kuwa lengo ni kuwafikia wananchi ili kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kujiunga na kuchangia kwenye Mfuko.

“Hili ni eneo ambalo lina fursa nyingi za kiuchumi, hivyo Mfuko tumeona tuwafikie wananchi hawa ambao ni mastaa wa mchezo kwenye shughuli zao za kila siku, ili waelewe huduma na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF,” alisema Bi. Witness.

Akifafanua zaidi, Bi. Witness alisema kujiunga na NSSF ni rahisi ambapo mwanachama anaweza kubofya *152*00# na kuchangia kuanzia shilingi 30,000 au zaidi kwa siku, wiki, mwezi au kulingana na msimu wa kipato.

Aliongeza kuwa mwanachama anayejiunga kwa ajili ya huduma za matibabu yeye pamoja na wategemezi wake yaani mke au mume na watoto wanne, anapaswa kuchangia shilingi 52,200 kwa mwezi ili kunufaika na matibabu kupitia mpango wa NSSF.

Kwa upande wake, Bw. Omar Nondo, mkazi wa Kiwangwa, alitoa shukrani kwa NSSF kwa kuwafikia wananchi wa eneo hilo na kutoa elimu ya hifadhi ya jamii.

“Naishukuru NSSF kutufikia katika eneo hili na kutupatia elimu ya hifadhi ya jamii. Kiukweli nimefurahi kujiunga ili niweze kuchangia na kunufaika na mafao yanayotolewa yakiwemo ya matibabu,” alisema Bw. Nondo.

NSSF imeendelea na kampeni hii ya utoaji wa elimu kwa lengo la kuongeza uelewa miongoni mwa Watanzania kuhusu hifadhi ya jamii na kuwahamasisha kujiunga ili waweze kujenga msingi wa maisha bora ya sasa na baadaye.