emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

KATIBU MKUU KIONGOZI WA ZANZIBAR ATEMBELEA BANDA LA NSSF KWENYE MKUTANO WA TAPA-HR JIJINI ARUSHA


Na MWANDISHI WETU, Arusha

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi wa Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) lililopo katika viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), kabla ya ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Utumishi wa Umma (TAPA-HR).

Mhandisi Zena alipata fursa ya kujionea namna ambavyo NSSF inavyotumia TEHAMA katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na wadau, hatua ambayo inawarahisishia wanachama kupata huduma za NSSF popote walipo kwa urahisi, haraka na uwazi.

Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo: “Mwelekeo Mpya wa Nafasi ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Kusukuma Mabadiliko Kuendana na Mageuzi ya Teknolojia ili Kuboresha Huduma kwa Wananchi.”

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Jumuiya ya TAPA-HR, AAPAM Tanzania na TPS-HRM. Jumuiya hizi zote zinatambulika rasmi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Lengo la mkutano huo ni kujadili na kuweka mikakati ya namna bora ya kuimarisha sekta ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala serikalini, hasa katika kipindi hiki cha mageuzi ya kidijitali, kwa manufaa ya utoaji huduma bora kwa wananchi.

MWISHO