emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

Naibu Waziri Mhe. Deus Sangu Apongeza NSSF kwa Uboreshaji wa Huduma Kupitia TEHAMA


Na MWANDISHI WETU, Arusha

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu, amepongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa hatua kubwa zilizopigwa katika utoaji wa huduma kupitia matumizi ya TEHAMA.

Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Utumishi wa Umma (TAPA-HR), uliofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha, Mhe. Sangu alisema NSSF imekuwa mfano wa kuigwa kwa kutumia TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wanachama.

Aidha, Mhe. Sangu alieleza kuwa uwekezaji wa NSSF katika maeneo yenye tija umeongeza ufanisi wa kifedha wa Mfuko, hivyo kuimarisha uwezo wake wa kuhudumia wanachama kwa wakati.

Aliwasihi waajiri kuhakikisha wanalipa michango kwa wakati ili kulinda ustawi wa wafanyakazi baada ya kumaliza mikataba yao ya ajira.

Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Bw. Josephat Komba, alimweleza Naibu Waziri kuwa huduma za NSSF zimeboreshwa kupitia mifumo ya TEHAMA, ambapo waajiri na wanachama wanaweza kupata huduma bila kufika ofisi za Mfuko.

Katika kilele cha mkutano huo, Mhe. Sangu alimkabidhi tuzo ya shukrani kwa NSSF, iliyopokelewa na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Rasilimali Watu na Utawala wa Mfuko, Bw. Ekwabi Mujungu. Tuzo hiyo ilitolewa kwa kutambua mchango wa NSSF katika kufanikisha mkutano huo.

Mkutano huo wa siku nne uliandaliwa kwa ushirikiano na jumuiya za TAPA-HR, AAPAM-TZ na TPS-HRM, unalenga kubadilishana uzoefu na kujadili nafasi ya wataalamu wa Rasilimali Watu na Utawala katika kuendana na mageuzi ya kiteknolojia.

MWISHO