News
MAONESHO YA KITAIFA YA KAZI ZA UTAMADUNI NA SANAA: FURSA KWA WASANII KUJIUNGA NA NSSF

Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ndg. Methusela Ntonda (kulia), akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Temeke, Bw. Feruzi Mtika (kushoto), ambapo alimweleza kuwa NSSF inaandikisha wanachama kutoka sekta rasmi pamoja na wananchi waliojiajiri kupitia Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi waliojiajiri. Alitembelea Banda la NSSF katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Mtika alimweleza Mgeni Rasmi kuwa NSSF imeanzisha Skimu hii, ambayo ni Mpango Maalum wa Kitaifa wenye lengo la kuwezesha wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu pamoja na huduma zinazotolewa na NSSF.
Aliongeza kuwa Maonesho ya Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa ni fursa kwa wasanii wote kujiunga na NSSF kwa ajili ya kutengeneza kesho yao iliyo njema, kwa kuwa sasa wana nguvu ya kufanya sanaa na ubunifu mbalimbali, lakini itafika kipindi watakapopungukiwa uwezo wa kufanya hivyo, na NSSF itakuwa mkombozi wao.
Mwisho alisema kuwa walengwa wa NSSF katika kundi la waliojiajiri ni pamoja na wanaojishughulisha na Sekta ya Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Uchimbaji Mdogo wa Madini, Usafirishaji (Bodaboda na Bajaji), pamoja na Biashara Ndogo Ndogo (Machinga, Mama/Baba Lishe, Ususi, wauza mkaa, wauza nyanya na wajasiriamali wengine wote).