emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YAENDELEA KUFUNGUA FURSA KWA VIJANA SAUT MWANZA KUPITIA KAMPENI YA ' WEKA TUWEKE' YA CLOUDS MEDIA*Wapatiwa elimu ya hifadhi ya jamii, waelezwa umuhimu wa kujiwekea akiba

Na MWANDISHI WETU,

Mwanza. Mamia ya wanafunzi wa Chuo cha SAUT cha jijini Mwanza wamepata elimu na kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kujiwekea akiba, kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Elimu hiyo imetolewa tarehe 16 Mei, 2024 na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya ikiwa ni kuelekea kilele cha Malkia wa Nguvu, Kanda ya Ziwa ambapo Mfuko ni moja ya wadau katika kampeni hiyo yenye fursa kwa makundi mbalimbali ambayo ni wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, wavuvi, wakulima, mama lishe, wafugaji na wajasiriamali wengine wote.

Bw. Mziya ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia NSSF. Amesema zipo faida nyingi anazonufaika nazo mwanachama wa NSSF ikiwemo ya kupata mafao mbalimbali likiwemo la matibabu ambalo hata wanafunzi wanaojiunga na kuchangia kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo watanufaika na fao hilo.

“Tunayo madirisha mawili ya kujiunga na NSSF moja ni la walioajiriwa kwa mujibu wa sheria na lingine ni wale ambao hawajaajiriwa wakiwemo wanafunzi. Mziya ameendelea kwa kusema wajasiriamali ambao hawajajiunga tunaendelea kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Vilevile ameendelea kusema kwamba, Mfuko umerahisisha huduma zake kwa kuweka kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA. Amesema kupitia mifumo ya TEHAMA waajiri wanaweza kutumia lango binafsi la mwajiri (Employer Portal) kwa ajili ya kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati na vilevile kwa upande wa wanachama (Member Portal) wanaweza kufuatilia taarifa zao popote walipo bila kulazimika kufika katika Ofisi za NSSF.

Amewataka wanachuo hao kuchangamkia fursa ya elimu ya hifadhi ya jamii waliyopatiwa na NSSF kwa ajili ya kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia kila mwezi. “Napenda kutoa rai kwa wanafunzi wa vyuo tumieni fursa ya elimu ya hifadhi ya jamii mliyopata kwa kujiunga na kujiwekea akiba NSSF kwa ajili ya kesho yenu iliyokuwa bora,” amesema Mziya.