emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​NSSF YAENDELEA KUTOA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KUPITIA JUKWAA LA MALKIA WA NGUVU


Na MWANDISHI WETU,

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kutumia majukwaa yenye ushawishi katika jamii kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, kwa lengo la kupanua wigo wa wananchi wanaopata huduma hizo, hususan wale waliojiajiri na wanaofanya shughuli zao mbalimbali.

Jukwaa la Malkia wa Nguvu ni miongoni mwa majukwaa muhimu yanayotumiwa na NSSF kufikisha elimu hiyo kwa wananchi, hususan wanawake, kwa kuwahamasisha kujiunga na kuchangia kupitia Hifadhi Skimu, mpango maalumu unaolenga kuwapatia watu waliojiajiri fursa ya kujihakikishia ulinzi wa kijamii na kiuchumi kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii.

Kupitia Hifadhi Skimu, wananchi wanaweza kujiunga na kuanza kuchangia kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi kwa kupiga *152*00#, kuchagua namba 9, kisha namba 6 na kufuata maelekezo yatakayotolewa.

Aidha, wanachama wanaochangia kwa miezi mitatu mfululizo wanastahili kunufaika na mafao ya matibabu, pamoja na mafao mengine yanayotolewa chini ya mpango huo kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.

Kwa kutumia majukwaa kama Malkia wa Nguvu, NSSF inaendelea kutekeleza azma yake ya kuhakikisha hifadhi ya jamii inawafikia wananchi wengi zaidi, bila kujali aina ya shughuli wanazofanya kiuchumi, huku ikiwahamasisha kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba na kujipatia ulinzi dhidi ya changamoto mbalimbali za maisha.

NSSF inaendelea kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa kila Mtanzania, kwa kuzingatia kuwa hifadhi ya jamii ni msingi muhimu wa ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu, katika kujenga maisha bora ya sasa na ya baadaye, sambamba na utekelezaji wa Dira 2050.

MWISHO