News
RC MTANDA APONGEZA JUHUDI ZA NSSF KUWAFIKIA WALIOJIAJIRI
Na Mwandishi Wetu
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa juhudi zake za kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi, hususan waliojiajiri, akisema hatua hiyo inaongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) unaoendelea jijini Mwanza, Mhe. Mtanda alisema NSSF imekuwa mstari wa mbele kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kujiunga na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kujiwekea akiba kwa
maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mhe. Gerson Msigwa, alitembelea banda la NSSF na kupongeza juhudi za Mfuko huo katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii.
Katika mkutano huo, Afisa Uhusiano Mkuu wa NSSF, Bw. Sebera Fulgence, akiwa mmoja wa wachangiaji mada iliyohusu “Kujenga Taswira Binafsi, Mawasiliano ya Kimkakati, Mauzo na Ushawishi kwa Umma kwa Ukuaji wa Taasisi katika Enzi ya Kidijitali” alielezea namna Wafanyakazi, na Taasisi zinavyoweza kutumia taswira (Branding), mikakati ya mawasiliano (Communication Strategy) na TEHAMA (ICT) jinsi vinavyoweza kurahisisha utoaji elimu na kuwafikia wadau wengi zaidi ktika zama hizi za kidigitali.
Ushiriki wa NSSF katika Mkutano wa TAGCO unaonesha dhamira ya Mfuko ya kusogeza huduma na elimu ya hifadhi ya jamii karibu zaidi na wananchi, hususan walio katia sekta rasmi na waliojiajiri, ili kuwawezesha kujiwekea akiba na kujenga uhakika wa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

