emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

WAMACHINGA ZAIDI YA 1,000 WAPATIWA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII


WAMACHINGA ZAIDI YA 1,000 WAPATIWA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII **NSSF yawahimiza kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na baadaye** Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam Zaidi ya wafanyabiashara wadogo 1,000 maarufu kama wamachinga wamepatiwa elimu ya umuhimu wa Hifadhi ya Jamii kupitia Hifadhi Skimu inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), katika mkutano ulioandaliwa na Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) uliofanyika Mei 6, 2026 katika Soko la Mwenge jijini Dar es Salaam. Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NSSF, Bw. Robert Kadege, alisema wananchi waliojiajiri wanapaswa kuona Hifadhi ya Jamii kama nguzo muhimu ya maisha yao, hasa wanapokumbana na changamoto au majanga mbalimbali. Alisema kupitia Hifadhi Skimu, mwananchi anayejiajiri anaweza kupata mafao mbalimbali ikiwemo matibabu, uzazi, uzee, urithi pamoja na msaada wa mazishi, jambo linalosaidia kulinda maisha na kipato cha familia hata pale nguvu ya kazi inapopungua. “Leo hii machinga naye ana nafasi ya kuwa na uhakika wa maisha yake ya baadaye. Kwa kiwango cha chini kinachoanzia Shilingi 30,000 kwa mwezi, mwananchi anaweza kuanza safari ya kujihakikishia usalama wa maisha yake na familia yake,” alisema Kadege. Aliongeza kuwa NSSF imeboresha mifumo ya TEHAMA inayomwezesha mwanachama kujisajili, kuchangia, kufuatilia michango yake na kupata huduma kwa urahisi akiwa popote alipo. Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Mbunde, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta isiyo rasmi ili wananchi waliojiajiri waweze kunufaika na huduma muhimu zikiwemo za Hifadhi ya Jamii. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIUMA, Bw. Ernest Matodo, alisema umachinga ni kazi halali inayolisha maelfu ya Watanzania, hivyo ni muhimu wafanyabiashara hao kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye kupitia NSSF. Baadhi ya wamachinga waliohudhuria mkutano huo walisema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa kuwa Hifadhi ya Jamii siyo kwa wafanyakazi wa serikali pekee, bali pia kwa wananchi wa kawaida wanaopambana kila siku kutafuta kipato. Katika mkutano huo, NSSF pia ilitoa huduma za papo kwa papo ikiwemo usajili wa wanachama wapya na elimu ya namna ya kujiunga na kuchangia kupitia simu za mkononi.