News
WANACHAMA WA NSSF WAFURAHIA HUDUMA BORA NA ELIMU KWENYE BANDA LA NSSF SABASABA.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wamefurahia kupata huduma mbalimbali muhimu pamoja na elimu kuhusu mafao na huduma mpya za Mfuko huo, baada ya kutembelea banda la NSSF lililopo kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa.
Banda la NSSF limeendelea kuvutia wananchi wengi na wanachama kutoka maeneo mbalimbali, huku wafanyakazi wake wakiwa wamejipanga kutoa huduma kwa haraka na kwa weledi.
Wanachama waliotembelea banda hilo walipata fursa ya kusajiliwa, kuhuisha taarifa zao, kuangalia michango yao, kufuatilia mafao yao, elimu kuhusu fursa za uwekezaji ikiwemo miradi ya nyumba na viwanja, namna Mfuko unavyopinga Rushwa na huduma za NSSF kidijitali kupita NSSF Portal.
Bi. Esther Mwakipesile, Mwanachama wa NSSF ambaye pia ni mfanyakazi wa sekta binafsi, alisema
“Nilifika hapa kutaka kujua kama mchango wangu unaendelea kuwasilishwa. Wameangalia taarifa zangu kwa haraka, na sasa nimeelewa kila kitu. Pia nimesajiliwa kwenye huduma ya NSSF kidijital, ni rahisi sana!”
Aidha, baadhi ya wananchi waliokuwa bado hawajajiunga na NSSF walipata fursa ya kujifunza umuhimu wa kujiunga na kuchangia NSSF, hasa wale waliojiajiri wenyewe kwenye maeneo mbalimbali.
Bw. Rashid Mtenga, mjasiriamali kutoka Temeka, alisema:
“Sikuamini kama watu tuliojiajiri tunaweza pia kuwa wanachama wa NSSF. Leo nimeelewa, na nimejiunga rasmi. Ni hatua muhimu kwa maisha ya baadaye.”
Kumbuka kuwa lengo la ushiriki wa NSSF katika Maonesho ya Sabasaba ni kuwasogezea huduma karibu wananchi na kuongeza uelewa kuhusu Hifadhi ya Jamii.