News
Wananchi Singida wahamasishwa kujiunga na kujiwekea akiba NSSF

Na MWANDISHI WETU,
Singida. Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gondwe, amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kujiunga na kujiwekea akiba katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia uchangiaji wa hiari kwa ajili ya kesho yao iliyo njema.
Mhe. Gondwe alisema hayo wakati akifungua kikao baina ya NSSF na Maafisa Maendeleo, Madiwani, viongozi wa masoko, maafisa wasafirishaji wa Halmashauri ya Singida pamoja na viongozi wa makundi mbalimbali ya wajasiliamali kuhusu umuhimu wa kujiunga na kujiwekea akiba kupitia mpango wa uchangiaji wa hiari ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa na NSSF.
Mkuu wa Wilaya huyo aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia NSSF kwa kuboresha mpango wa uchangiaji wa hiari unaowawezesha Watanzania wote waliojiajiri kujiunga na kuchangia NSSF kuanzia shilingi 30,000 ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu.
Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Bw. Oscar Kalimilwa alisema lengo la semina hiyo ni kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri wenyewe, ambao baada ya kujiunga wanaweza kujichangia kidogo kidogo kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Vitunguu Singida, Bw. Iddy Mwanja alisema elimu ya hifadhi ya jamii waliyoipata katika semina hiyo wataenda kuisambaza kwa wengine ili waweze kuelewa umuhimu wa kujiunga na NSSF na kujiwekea akiba.