News
WANANCHI WAMIMINIKA KUNUNUA SUKARI YA MKULAZI NA BIDHAA ZA SISALANA KATIKA MAONESHO YA SABASABA

WANANCHI WAMIMINIKA KUNUNUA SUKARI YA MKULAZI NA BIDHAA ZA SISALANA KATIKA MAONESHO YA SABASABA
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam. Ujio wa Sukari ya Mkulazi pamoja na bidhaa za kiwanda cha Sisalana katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) umekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wengi. Wateja wamekuwa wakivutiwa na bei nafuu za bidhaa hizo, zinazouzwa kwa gharama inayomudu kila Mtanzania.
Sukari hiyo inazalishwa na kiwanda cha Mkulazi kinachomilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza. Kiwanda hiki kilizinduliwa rasmi mwezi Agosti, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama sehemu ya juhudi za kupunguza nakisi ya sukari nchini.
Bi. Rose Jeremia, mkazi wa Dar es Salaam, alielezea furaha yake alipojionea bidhaa hizi katika banda la NSSF namba 13: “Nilikuja hapa Sabasaba kwa ajili ya kujionea vitu vizuri vilivyopo, lakini nilipopita niliona sukari inauzwa kwa bei rahisi. Nikavutiwa, na nikachukua kwa sababu inaonekana ni nzuri na bei ni rafiki kwa kila Mtanzania,” alisema Bi. Rose.
Bi. Rose aliwataka wananchi wengine wanaotembelea maonesho hayo, kufika katika banda la NSSF ili waweze kujipatia sukari ya Mkulazi kwa bei nafuu.
Naye Bi. Magdalena Njaidi, mkazi wa Mapinga, Bagamoyo, alielezea furaha yake alipojivunia kununua kiti kilichotengenezwa na kiwanda cha Sisalana kilichomilikiwa na NSSF: “Nimenunua kiti hiki, ni fahari ya Tanzania. Kimetengenezwa hapa Tanzania na ni cha ubora wa hali ya juu. Naenda kukitumia nyumbani. Naomba wananchi wengine wanaotembelea Sabasaba, wasikose kutembelea banda hili ili wapate bidhaa bora kabisa,” alisema Bi. Magdalena.
Kwa upande wake, Bw. Naby Adonis, Afisa Mauzo na Masoko wa kiwanda cha Mkulazi, alielezea kuhusu bidhaa za sukari zinazopatikana katika banda la NSSF: “Sukari yetu inapatikana kwa ujazo wa kilo moja, kilo 25 na kilo 50. Tunaendelea kuuza kwa bei nafuu sana, hivyo tunawakaribisha wananchi wote watembelea banda letu ili kujipatia sukari bora,” alisema Bw. Adonis.