News
MKURUGENZI MKUU WA NSSF ATOA UZOEFU WA MFUKO HUO KATIKA KUCHANGIA MAENDELEO YA KIJAMII NCHINI

MKURUGENZI MKUU WA NSSF ATOA UZOEFU WA MFUKO HUO KATIKA KUCHANGIA MAENDELEO YA KIJAMII NCHINI
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba, amewasilisha mada ya uzoefu wa NSSF katika kuendesha maendeleo ya Uchumi wa kijamii kupitia ufadhili wa ujenzi wa miundombinu na ushughulikiaji wa sekta ya wananchi waliojiajiri, katika mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Moja ya miradi mikubwa ya mfano ambayo NSSF imewekeza katika ujenzi wa miundombinu ni ujenzi wa Daraja la Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa watanzania hususan wale wanaokwenda na kurudi Kigamboni.
Mkutano huo ulifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambaye aliwahimiza wataalamu wanaohudhuria mkutano huo kuandaa mikakati ya jinsi gani Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaweza kuchangia katika kuongeza juhudi zinazoendelea za kuongeza ufadhili wa uwekezaji katika miundombinu ya kijamii na kiuchumi maeneo ya vijijini.
Amesema uwekezaji katika miundombinu ya vijijini utasaidia kuongeza tija na ubora wa maisha katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji, kutengeneza ajira na kupunguza uhamaji wa wananchi kutoka vijini kwenda mijini.
Mkutano huo wa siku mbili umebeba kaulimbiu isemayo “Sekta ya Hifadhi ya Jamii; Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu kwa ajili ya masuala ya Kiuchumi na Kijamii katika Bara la Afrika.” Ukiwakutanisha washiriki kutoka 15 za Bara la Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Sudan Kusini, Comoro, Cote d'ivoire, Gambia, Sierra Leone, Mali, Namibia na mwenyeji Tanzania.