News
NSSF UBUNGO YAWAJENGEA UWEZO WAAJIRI WA SEKTA BINAFSI

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia Ofisi ya Mkoa wa Ubungo umeendesha semina maalumu kwa waajiri wa sekta binafsi, yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu wajibu wao wa kuandikisha na kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Ubungo, Bw. Joseph Fungo, alisema semina hiyo imelenga kuhakikisha waajiri wanapata elimu ya kina kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Mfuko, hususan usajili sahihi wa wafanyakazi, uwasilishaji wa michango kwa wakati, na matumizi ya mfumo wa NSSF Portal—hasa sehemu ya Employer Portal—kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na uwazi.
Bw. Fungo aliwahimiza waajiri kutimiza wajibu wao kikamilifu na kuepuka vitendo vyovyote vya udanganyifu vinavyoweza kudhoofisha sifa ya kampuni au kuathiri haki za wafanyakazi. Aidha, alisisitiza kuwa NSSF itaendelea kushirikiana na waajiri ili kuhakikisha ustawi wa jamii ya wafanyakazi unalindwa kwa mujibu wa sheria.
Katika semina hiyo, NSSF ilisisitiza umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijitali ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma kwa waajiri. Waajiri walifundishwa namna bora ya kutumia mfumo wa Employer Portal ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao moja kwa moja bila kulazimika kufika ofisini, hatua inayookoa muda na kupunguza gharama.
Semina hiyo ilipokelewa kwa hamasa kubwa, ambapo waajiri walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupata majibu ya kina kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa NSSF.