News
NSSF YAPANUA UELEWA WA HIFADHI YA JAMII KUPITIA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA UCHUKUZI

Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeshiriki katika Kongamano la Tatu la Kimataifa la Uchukuzi na Usafirishaji linalofanyika katika Viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21 Agosti, 2025.
Kongamano hilo limefunguliwa rasmi na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), likiwa na kauli mbiu isemayo “Tumia mfumo bunifu na endelevu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa sekta ya usafirishaji.” Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Katika kongamano hilo, NSSF inatoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa washiriki kuhusu mafao yanayotolewa na Mfuko, kuandikisha wanachama wapya kutoka sekta binafsi na wananchi waliojiajiri, pamoja na kuelimisha namna ya kujichangia kupitia simu ya kiganjani.
Aidha, NSSF inatangaza fursa za uwekezaji katika miradi ya nyumba na viwanja, sambamba na kutoa elimu juu ya huduma za mifumo ya kidijitali ikiwemo Lango la Huduma (NSSF Portal).
Kupitia ushiriki huu, NSSF inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko, na kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kujenga taifa lenye usalama wa kijamii na kiuchumi.