emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

MKUTANO WA 57 WA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI WA MFUKO WA TAIFA WA HIFADHI YA JAMII (NSSF)


Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kukua baada ya thamani ya NSSF kupanda kutoka shilingi trilioni 9.8 hadi kufikia shilingi trilioni 11.4, hatua inayoonesha ongezeko kubwa la thamani ya rasilimali za NSSF.

Hayo yameelezwa wakati wa Mkutano wa 57 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF uliofanyika mkoani Morogoro, ukiwa na lengo la kujadili maendeleo ya Mfuko pamoja na masuala yanayohusu ustawi wa wafanyakazi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Zuhura Yunus, amesema NSSF imepiga hatua katika ukuaji wa thamani yake, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya viongozi na wafanyakazi ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kukua na kufikia malengo yake.

Aidha, ameipongeza NSSF kwa kuendelea kuyafikia makundi mbalimbali ya wananchi waliojiajiri huku akitoa rai kwa NSSF kuendelea kuyafikia zaidi makundi hayo kwani hifadhi skimu ni nguzo muhimu ya mustakabali wa hifadhi ya jamii nchini, akibainisha kuwa Serikali inalenga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi, hususan waliojiajiri, wanajumuishwa katika mfumo huo.

"Nimpongeze Mkurugenzi Mkuu, menejimenti na wafanyakazi kwa mafanikio mliyopata pamoja na kupata ithibati ya kimataifa. Maeneo ya vipaumbele vya mkakati wa nane, matumizi ya Tehama, kuimarisha mawasiliano yenye kimkakati ni mambo muhimu," alisema Bi. Yunusi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, akitoa ufafanuzi wa awali amesema misingi ya utawala bora inayotekelezwa ndani ya NSSF imekuwa miongoni mwa sababu zinazosaidia kufikia malengo yaliyowekwa.

Aidha, aliongeza kuwa Juni mwaka huu Mfuko umepata ithibati ya ubora katika utoaji huduma, ithibati hii si kwa mujibu wa viwango vya Tanzania tu bali pia viwango vinavyotambulika kimataifa yaani (ISO 2001:2015). "Utawala bora na usimamizi wa rasilimali fedha na watu umetupa hati safi kwa miaka yote. Tumekuwa tukipata vyeti kadhaa ikiwa ni pamoja na kutambuliwa na TRA kama mlipa kodi mkubwa. Wenzetu wa Serikali Mtandao (EGA) wametuona na kututambua kama taasisi kiongozi katika taasisi zinazofuata na kutumia masuala ya teknolojia," alisema.

Katika jitihada za kufikia Watanzania milioni 3.7 waliojiajiri, Mfuko umetengeneza kanzi data ya baba lishe na mama lishe yenye idadi ya wanachama zaidi ya milioni 34. Kundi hili Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye mlezi na sisi kama Mfuko tumejipanga kuwahudumia vyema ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunawasajili na pia wanapata mafao. “Ni kwa mara ya kwanza katika nchi yetu kuona watu waliojiajiri wanapata haki sawa na wale walioajiriwa, na wakifikisha vigezo wanalipwa mafao sawa” alisema Mshomba.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira bora na wezeshi ya ufanyaji kazi, uwekezaji pamoja na biashara, jambo lililochochea ongezeko la wanachama na uimara wa mifumo ya hifadhi ya jamii.

Aidha ametoa wito kwa waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati kwani kwa kufanyan hivyo ni wajibu wa kisheria unaolenga kulinda haki za wafanyakazi.

Mwakilishi wa Wafanyakazi, Bw. Materu Maneja wa NSSF Kinondoni, alitoa shukrani kwa mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko na kwa maelekezo mazuri aliyoyatoa. Alisema wafanyakazi wamepokea pongezi za ukuaji wa Mfuko na ithibati, na wataendelea kupambana kuhakikisha wanafikia malengo.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali na Utawala wa NSSF, Bw. Ekwabi Mjungu, aliwakaribisha wajumbe wote na kuwaomba wakumbuke wafanyakazi waliotangulia mbele za haki. Aliwahakikishia wajumbe uwepo wa maandalizi mazuri na mazingira safi ya kikao, na kuwashukuru kwa kufika kwa wakati.

Kikao hicho cha 57 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF kimehitimisha jana tarehe 28 mkoani Morogoro kwa azimio la pamoja la kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuimarisha ushirikiano na wadau, na kuhakikisha kuwa NSSF inakuwa taasisi bora zaidi katika kutoa huduma za hifadhi ya jamii nchini Tanzania.