emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

MKUU WA MKOA WA TANGA AFURAHISHWA NA UBORESHAJI WA MIFUMO YA UTOAJI HUDUMA NSSF


*Ni katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 kilichofanyika Tanga

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Batilda Burian, amepongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa jitihada zake za kuboresha mifumo ya utendaji kazi na utoaji huduma kwa wateja, akieleza kuwa maboresho hayo yamechangia kuimarika kwa utendaji wa Mfuko na kuongeza thamani yake.

Akizungumza wakati wa kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja kilichofanyika katika Ofisi za NSSF Mkoa wa Tanga, chini ya kaulimbiu ya “Huduma Bora kwa Vitendo,” Bi. Burian amesema uboreshaji wa mifumo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wateja wanapata huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi mahitaji yao.

Amesema jitihada hizo zinaonesha dhamira ya NSSF katika kuimarisha mifumo yake ya utendaji na usimamizi wa ubora, hatua iliyochangia pia kupatikana kwa cheti cha usimamizi wa ubora cha kimataifa cha ISO 9001:2015.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amekabidhi vyeti vya pongezi kwa watumishi waliofanya vizuri zaidi katika utoaji wa huduma kwa wateja, ikiwa ni sehemu ya kutambua juhudi zao na kuhamasisha utendaji bora, uwajibikaji na weledi katika kuwahudumia wateja.

Vilevile, vyeti vilitolewa kwa waajiri wanaozingatia sheria na taratibu za hifadhi ya jamii kwa kuhakikisha michango ya wafanyakazi inawasilishwa kwa wakati.

Maadhimisho hayo yanaonesha dhamira ya NSSF ya kutafsiri kaulimbiu ya “Huduma Bora kwa Vitendo” kuwa matokeo halisi kupitia maboresho ya mifumo, kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha ushirikiano na wadau wake.

NSSF inaendelea kuhimiza utamaduni wa kutoa huduma bora, kwa kuzingatia mahitaji ya wateja na kuhakikisha kuwa wanachama, waajiri na wadau wengine wanapata huduma zenye ubora na ufanisi.