emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​NSSF YAPOKEA UJUMBE WA CNPS KUTOKA CÔTE D’IVOIRE KWA ZIARA YA MAFUNZO KUHUSU MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA HUDUMA KWA WANACHAMA NA WASTAAFU


Dar es Salaam, Tanzania

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepokea ujumbe kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa Côte d’Ivoire (CNPS), uliofika nchini kwa ziara ya mafunzo yenye lengo la kujifunza matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususan teknolojia ya bayometriki katika uhakiki wa wanachama, wastaafu na wanufaika.

Ujumbe huo uliongozwa na Bwana Essoua Kouadio Yves na ulipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bwana Ibrahim Maftah, akifuatana na Mkurugenzi wa TEHAMA, Bwana Donald Mhaiki, Meneja wa Mifumo, Bwana Mihayo Mathayo, pamoja na maafisa kutoka Kurugenzi ya TEHAMA na watumishi wa maeneo ya mafao na matibabu.

Wakati wa ziara hiyo, ujumbe wa CNPS ulipata maelezo kuhusu matumizi ya teknolojia ya bayometriki, ikiwemo alama za vidole na utambuzi wa sura, katika usajili na uhakiki wa wanachama, uthibitishaji wa taarifa za wastaafu na wanufaika, pamoja na kuwezesha utoaji wa mafao. Aidha, wageni walipata fursa ya kujionea mifumo hiyo ikifanya kazi kwa vitendo na kubadilishana uzoefu kuhusu mafanikio, changamoto na fursa za kuboresha huduma kupitia TEHAMA.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Meneja wa Mifumo wa NSSF, Bwana Mihayo Mathayo, alieleza kuwa matumizi ya teknolojia ya bayometriki yamechangia kuimarisha usalama na uaminifu wa taarifa za wanachama, kupunguza uwezekano wa udanganyifu na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama, wastaafu na wanufaika.

Kwa upande wake, Bwana Essoua Kouadio Yves aliishukuru NSSF kwa mapokezi mazuri na utayari wa kushirikiana na ujumbe huo. Alieleza kuwa mafunzo na uzoefu walioupata vitakuwa na mchango muhimu katika kuboresha mifumo ya uhakiki na utoaji wa huduma za hifadhi ya jamii nchini Côte d’Ivoire.

Ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi na kubadilishana maarifa na uzoefu miongoni mwa mifuko ya hifadhi ya jamii barani Afrika, kwa lengo la kuboresha mifumo ya TEHAMA na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanachama na wastaafu.