emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA PILI WA DOHA DIALOGUE


Na. OWM(KAM), Dar es Salaam.

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue kuhusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5 na 6, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, huku Serikali ikieleza kuwa mkutano huo utatoa fursa ya kufungua zaidi milango ya ajira kwa Watanzania nje ya nchi.

Mkutano huo utafanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency na utawakutanisha wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), nchi za Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC), ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, pamoja na Jordan na Lebanon.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema Tanzania imepewa nafasi hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika ndani ya bara la Afrika.

“Tanzania ni nchi ya pili kuwa mwenyeji wa Doha Dialogue, mkutano huo ambao unafanyika kila baada ya miaka miwili. Kwa mara ya kwanza unafanyika ndani ya bara la Afrika na Tanzania imepata nafasi ya kuwa mwenyeji,” alisema.

Aidha, Mgeni Rasmi katika mkutano huo utakaokutanisha zaidi ya nchi 33 anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Waziri Sangu, Mkutano wa Kwanza wa Doha Dialogue ulifanyika Doha, Qatar, Mei 21 na 22, 2024, ukihusisha nchi 33, zikiwamo 25 za Afrika, nchi za Ghuba pamoja na Jordan na Lebanon.

Alisema Tanzania ilishiriki katika mkutano huo na miongoni mwa matokeo yake ilikuwa kupitishwa kwa azimio lililojulikana kama Doha Declaration, lililoweka misingi ya kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nchi za Kiarabu kuhusu uhamaji wa nguvu kazi.

Waziri Sangu amesema mkutano wa mwaka huu utajadili maeneo mbalimbali, ikiwamo uimarishaji wa mikataba ya ajira baina ya nchi, maarufu kama Bilateral Labour Migration Agreements, uanishaji wa ujuzi wa wafanyakazi na mahitaji ya soko la ajira.

Alisema pia washiriki watajadili namna ya kujenga mifumo ya uhamaji wa nguvu kazi inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji mapya ya soko la ajira, huku ikihakikisha wafanyakazi wanapata ajira zenye staha.

Alisema mkutano huo utatoa fursa kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhamaji wa nguvu kazi, kupanua fursa za ajira nje ya nchi, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika na GCC+.

“Katika mkutano huu tutawaonyesha wenzetu namna ambavyo kama nchi tumejipanga na namna Serikali ilivyotengeneza mazingira kwa vijana ili waweze kuchangamkia fursa za ajira kutoka nchi mbalimbali,” alisema.

Mkutano huu umebeba kaulimbiu isemayo: “Kutoka Ahadi hadi Vitendo: Kuendeleza Uhamaji wa Nguvu Kazi wenye Haki na Endelevu wa Nchi za Afrika na Ghuba (CCC+).”