emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

WAZIRI MKUU MSTAAFU, MHE. PINDA ATEMBELEA NSSF KATIKA MAONESHO YA NANE NANE, DODOMA


WAZIRI MKUU MSTAAFU, MHE. PINDA ATEMBELEA NSSF KATIKA MAONESHO YA NANE NANE, DODOMA

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda ametembelea Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hiyo pamoja na Taasisi zake ikiwemo NSSF. Maonesho ya Nanenane 2025 Kitaifa yanaendelea katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma ambapo kilele chake ni tarehe 8 Agosti 2025.

Akitoa maelezo mbele ya Mhe. Pinda, Meneja wa NSSF Mkoa wa Dodoma,Yahya Mudhihir, alieleza namna ambavyo NSSF imeboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kidijitali, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama na wadau.

Alisema kwa sasa mwanachama anaweza kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na NSSF bila kulazimika kufika ofisini, ikiwemo, usajili wa wanachama wapya kupitia mfumo ya kidijitali, uwasilishaji na ukusanyaji wa michango ya waajiri na wanachama na kulipa mafao mbalimbali.

Aliongeza kuwa NSSF inashiriki maonesho haya kwa lengo la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii ikiwemo elimu kuhusu mafao, jinsi ya kujisajili wanachama wapya kutoka sekta binafsi na wananchi waliojiajiri, elimu kuhusu kujichangia kupitia simu ya kiganganjani popote walipo, pia kutangaza fursa za uwekezaji katika miradi ya nyumba na viwanja, elimu kuhusu huduma za Mifumo mbalimbali ikiwemo Lango la Huduma (NSSF Portal) pamoja na elimu ya mapambano dhidi ya Rushwa.

Aidha, alimweleza Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Pinda kuwa NSSF katika kutanua wigo wake wa uwekezaji, umewekeza katika mradi wa kimkakati ambao ni Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ambacho ni ubia na Jeshi la Magereza

Kwa upande wake Mhe. Pinda alisema kuwa Kiwanda cha Sukari Mkulazi ni ushahidi wa namna taasisi za Serikali zinavyoweza kuwekeza katika miradi yenye tija kwa taifa hasa kwa kutumia rasilimali zao ili kuboresha maisha ya Watanzania, kukuza uchumi wa taifa na kuleta mapinduzi ya viwanda.