emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF Yaanza Awamu ya Pili ya Kampeni Staa wa Mchezo Paka rangi, Yaunga Mkono Ajenda ya Nishati Safi ya Rais Samia


*Balozi Siro Apongeza Kuwafikia Waliojiajiri Na MWANDISHI WETU, Kigoma. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanza awamu ya pili ya kampeni ya Staa wa Mchezo Paka Rangi mkoani Kigoma, huku Mkuu wa Mkoa, Balozi Simon Siro, akimpongeza Mfuko kwa kuunga mkono ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi. Hii imefanyika kupitia ugawaji wa majiko ya gesi kwa mama lishe, baba lishe na wastaafu mkoani humo. Akizungumza Septemba 25, 2025, katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi za NSSF Kigoma, Balozi Siro alisema hatua hiyo ni ushahidi wa dhahiri kuwa NSSF haitekelezi tu majukumu yake ya msingi, bali pia inagusa maisha ya wananchi kwa matendo. “Nawashukuru sana NSSF kwa kazi kubwa mnayofanya. Kitendo cha kuleta mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Kigoma na kurudisha kwa jamii kupitia kampeni ya Staa wa Mchezo Paka Rangi, kwa kutoa majiko ya gesi, kinaonesha mmebeba ajenda ya Rais wetu ambaye ni kinara wa nishati safi,” alisema Balozi Siro. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema kampeni hii inalenga kuhakikisha wananchi waliojiajiri wanajiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao yanayotolewa na Mfuko. “Tumewawekea wananchi urahisi wa kuchangia kadri ya kipato chao; iwe ni kwa siku, wiki, mwezi au msimu kulingana na shughuli zao. Lengo letu ni kuhakikisha kundi kubwa la waliojiajiri linapata hifadhi ya jamii,” alisema Bw. Mshomba. Aidha, Bw. Mshomba alibainisha kuwa msaada wa majiko ya gesi ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia katika kusimamia matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira na afya za wananchi. Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. James Oigo, alisema kampeni ya Staa wa Mchezo Paka Rangi inawahamasisha waajiri na wanachama waliojiajiri kuendelea kulipa michango yao kila mwezi, ili kupata mafao yanayojumuisha kinga ya matibabu na mafao mengine. Baadhi ya wanufaika wa msaada huo, akiwemo Sheikh Mramba Mussa, baba lishe, na mama lishe Ester Sungura, waliishukuru NSSF kwa msaada huo na kuhamasisha wenzao kujiunga na Mfuko. “Majiko haya ya gesi yatatusaidia sana katika kazi zetu. Tunawahimiza wajasiriamali wote wajiunge na NSSF kwa kuwa manufaa yake ni makubwa, ikiwemo kupata mafao ya matibabu,” alisema Ester Sungura. Hatua hii ya NSSF imetajwa kuwa chachu ya kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika hifadhi ya jamii, huku ikibeba ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi.