emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​NSSF YAKABIDHI MAJIKO JANJA KUUNGA MKONO AJENDA YA NISHATI SAFI



Makunduchi, Zanzibar, Agosti 12, 2026

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umekabidhi majiko janja 10 katika Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.

Majiko hayo yanalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha afya za wananchi na kuinua ustawi wa jamii.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, Mhe. Wannu Hafidhi Ameir, alipokea majiko hayo ambayo yatakabidhiwa katika shule za sekondari.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mhe. Wannu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), aliishukuru NSSF na wadau wengine kwa kuunga mkono juhudi za taasisi hiyo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

"Naamini huu ni mwanzo tu. Tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinatumia nishati safi. Tunawashukuru NSSF na wadau wengine kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana nasi katika kuwahudumia wananchi," alisema Mhe. Wannu.

Alisema msaada na vifaa vilivyotolewa na wadau mbalimbali vitawanufaisha wananchi wa Makunduchi na Wilaya ya Kusini kwa ujumla, ambapo madaftari yatagawiwa katika shule za msingi, vitabu vitapelekwa shule za sekondari, majiko ya gesi yatatolewa kwa vikundi vya wanawake, huku majiko janja yaliyotolewa na NSSF yakitarajiwa kuboresha huduma za upishi katika shule.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema ushiriki wa Mfuko huo ni sehemu ya kuunga mkono ajenda ya Taifa ya matumizi ya nishati safi inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sambamba na kuendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi, hususan waliojiajiri.

“NSSF inaamini kuwa matumizi ya nishati safi ni uwekezaji katika afya za wananchi, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu. Tumekabidhi majiko 10 kama sehemu ya mchango wetu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini,” alisema Bw. Mshomba.

Alieleza kuwa, pamoja na kukabidhi majiko hayo, NSSF imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia katika Mfuko kupitia Skimu ya Hifadhi, inayowawezesha kupata mafao mbalimbali ikiwemo pensheni ya uzee, pensheni ya ulemavu, pensheni ya urithi, mafao ya uzazi, matibabu na huduma nyingine zinazotolewa na Mfuko huo.

Bw. Mshomba alisema matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda afya za wananchi dhidi ya madhara ya moshi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo salama, kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya jamii.

“Majiko haya ni mwanzo wa ushiriki wetu katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na elimu pamoja na teknolojia ya nishati safi,” alisema.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, aliipongeza Taasisi ya MIF kwa kuandaa Tamasha la Kizimkazi, akisema limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Alisema juhudi hizo zinaendana na dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza matumizi ya nishati safi nchini na barani Afrika, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kutumia teknolojia zinazolinda mazingira na kuboresha afya zao.

Ugawaji wa majiko hayo unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia ushirikiano wa Taasisi za Serikali na Binafsi. NSSF na wadau mbalimbali wamekuwa mstari mbele kuunga mkono juhudi hizo huku wananchi wakiendelea kunufaika na elimu kuhusu hifadhi ya jamii na huduma zinazotolewa na Mfuko huo.