News
NSSF Yatoa Elimu ya Hifadhi ya Jamii Katika Kongamano la Madini
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuimarisha juhudi za kuwafikia wananchi waliojiajiri kwa kutoa elimu ya hifadhi ya jamii katika Kongamano la Madini , katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SabaSaba).
Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa.
Elimu hiyo ilitolewa na Meneja wa Sekta ya Waliojiajiri wa NSSF, Bi. Rehema Chuma, kwa kushirikiana na Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Bw. Winniel Lusingu, ambapo walifafanua manufaa ya uanachama wa NSSF kwa wananchi waliojiajiri, hususan wachimbaji wadogo wa madini.
Katika elimu hiyo, waliwahimiza wachimbaji na wananchi wengine waliojiajiri kutumia fursa ya kujiunga na NSSF na kuendelea kuchangia ili kujijengea hifadhi ya kipato kwa maisha ya baadaye pamoja na kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko, ikiwemo pensheni, mafao ya urithi, ulemavu na mafao mengine yanayostahili kwa mujibu wa sheria.
Aidha, walisisitiza kuwa hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu ya ustawi wa wananchi na kwamba kujiunga mapema na kuendelea kuchangia kutawawezesha wananchi waliojiajiri kujenga mustakabali wenye uhakika kwao na familia zao.
Mwisho

