emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YATUNUKIWA CHETI CHA MSHIRIKI BORA KATIKA UTOAJI ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KWA WAJASIRIAMALI KWENYE MAONESHO YA JUA KALI/NGUVU KAZI – KIGALI, RWANDA


Na Mwandishi Wetu

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetunukiwa cheti cha mshiriki bora katika utoaji wa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali katika Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki, maarufu kama Jua Kali – Nguvu Kazi, yaliyofanyika katika Viwanja vya Gikondo, Kigali, Rwanda.

Katika maonesho hayo, Tanzania imeibuka mshindi na kupata tuzo nne kati ya sita, ambapo wajasiriamali wa Tanzania waliibuka washindi katika makundi mbalimbali, huku NSSF ikitambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika kuwaelimisha wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii na kuchangia ili kuhakikisha uhakika wa kipato na maisha bora baada ya kustaafu.

Akizungumza katika kilele cha maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, Juan Haguma, amesema Serikali ya Rwanda imefarijika kuona wajasiriamali zaidi ya 2,000 wakishiriki kuonesha na kufanya biashara, hatua inayokuza uchumi na kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ushindi huu wa Tanzania, ikiwemo kutambuliwa kwa NSSF, unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali na taasisi zake katika kuendeleza sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati, huku ikihakikisha kuwa wajasiriamali hao wanapata elimu na huduma stahiki za hifadhi ya jamii.

Maonesho hayo ya Jua Kali – Nguvu Kazi yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kubadilishana uzoefu na teknolojia, pamoja na kukuza biashara baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.