News
Naibu Waziri Dkt. Evaline Munisi Atembelea Banda la NSSF SabaSaba, Apongeza Elimu ya Hifadhi ya Jamii
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Evaline Wilbard Munisi, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Dkt. Munisi amepongeza juhudi zinazofanywa na NSSF za kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi.
NSSF inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii, ikiwemo mafao ya wanachama, uandikishaji wa wanachama wapya kutoka sekta binafsi na wananchi waliojiajiri, pamoja na namna rahisi ya kujiandikisha popote walipo. Aidha, wananchi wanapata elimu kuhusu uwekezaji wa NSSF katika miradi ya nyumba na viwanja.
Pia, NSSF inaendelea kutoa elimu kuhusu huduma za kidijitali, ikiwemo Lango la Huduma la NSSF (NSSF Portal), na kuwahamasisha wanachama kutumia mifumo ya kidijitali ya Mfuko ili kupata huduma mbalimbali kwa urahisi, zikiwemo kuangalia taarifa za michango, kulipia michango na kufungua madai.

