emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

MAKALA AWAONYA WAVAMIZI WA ARDHI MABWEPANDE


*Asema Serikali imedhamiria kuyarudisha kwa wenye maeneo yote, aipongeza NSSF kwa kupima vizuri ardhi yake na kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule

Na MWANDISHI WETU

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala ameridhishwa na utaratibu mzuri uliochukuliwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa kupima viwanja katika ardhi ya Mfuko ambayo ilikuwa imeanza kuvamiwa na wavamizi wa ardhi katika shamba lake lililopo Kata ya Mabwepande Wilaya ya Kinondoni.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mabwepande, Mhe. Makala alisema katika kata hiyo baadhi ya wavamizi wa ardhi walivamia maeneo ya watu pamoja na yanayomilikiwa na taasisi za Serikali ikiwemo NSSF, DDC na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuanza kukata viwanja ambavyo waliviuza kwa watu wengine kinyume cha sheria.

Mhe. Makala alisema kutokana na migogoro ya ardhi iliyokithiri katika Kata ya Mabwepande aliunda kamati ambayo ilifanya kazi kwa siku 78 ambapo zaidi ya wananchi 3,928 waliwasilisha nyaraka zao mbele ya kamati hiyo ambapo waliovamia katika eneo la NSSF walishindwa kutoa uthibitisho wowote hivyo waliondolewa na ardhi hiyo ilirudishwa kwa mmiliki ambaye ni NSSF.

“Nasikia NSSF tayari ameshalipima eneo lake ambalo analimiliki kisheria na ameshakata viwanja ambapo nilimuelekeza aweke bei rafiki ili wananchi waweze kununua jambo ambalo ametekeleza na pia ametoa mita za mraba 10,000 ambazo zitajengwa shule,” alisema.

Mhe. Makala alisema NSSF wanapaswa kuuza viwanja katika eneo lao ili kuepusha wavamizi wasije kuvamia tena katika eneo hilo kwani Serikali imedhamiria kuyarudisha maeneo yote yaliyovamiwa katika Kata ya Mabwepande ambapo wameanza katika eneo la NSSF na sasa wanaenda katika eneo la DDC na baadaye katika eneo la Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo lengo ni kuhakikisha wavamizi wote wanaondolewa.

Alizitaka taasisi zote zinazomiliki ardhi katika Kata ya Mabwepande zifike katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ili waweze kuanza kuyatambua maeno yao na kuyapima, na kwamba kila mvamizi wa ardhi anapaswa kutoa ushirikiano kwani hayo ndio maelekezo na maagizo ya Serikali.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Gondwe alisema miongoni mwa maeneo ambayo yalivamiwa ni eneo la NSSF lakini wavamizi hao wamekimbia na tayari eneo hilo limeshapimwa viwanja na Mfuko umetoa eneo ambalo litajengwa shule ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwahakikishia watoto wa Kitanzania wanasoma karibu na maeneo yao.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge aliupongeza Mfuko wa NSSF kwa kuamua kulipima eneo lake ambalo lilianza kuvamiwa na wavamizi wa ardhi.