emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

MAKAMU WA RAIS MHE. DKT. MPANGO AFURAHISHWA NA ‘HIFADHI SCHEME’ YA NSSF


MAKAMU WA RAIS MHE. DKT. MPANGO AFURAHISHWA NA ‘HIFADHI SCHEME’ YA NSSF

*Ni wakati alipotembelea banda la NSSF kabla ya ufunguzi

Na MWANDISHI WETU,

Arusha. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amefurahishwa na ‘Hifadhi Scheme’ kwa Wananchi waliojiajiri wakati alipotembelea banda la NSSF, katika ufunguzi wa Kongamano la 14 la Kimataifa la Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika.

“Ninalifurahia sana jambo hili kwa sababu nchi yetu watu waliojiajiri wapo wengi hasa vijana, nawapongeza sana NSSF,” alisema Mhe. Dkt. Mpango.

Wakati wa ufunguzi, Mhe. Dkt. Mpango alisema pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika kutumika kuwekeza katika kuendeleza miundombinu ni vema kuhakikisha michango ya wanachama ambayo imetengwa kama kinga dhidi ya misukosuko ya kiuchumi na kijamii pamoja ba kukabiliana na umasikini inabaki kuwa ya kutosha kukidhi malengo ya msingi ya uanzishwaji wake.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, alimweleza Makamu wa Rais kuwa kupitia skimu hiyo, NSSF inasajili wananchi waliojiajiri wakiwemo mama lishe, boda boda na wananchi wengine waliojiajiri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alimueleza Makamu wa Rais kuwa wananchi wanaifurahia ‘Hifadhi Scheme’ na wanajiunga kwa wingi kwa ajili ya kujiwekea akiba ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF yakiwemo ya matibabu.

Mkutano huo umewakutanisha wadau, watunga sera, wasimamizi na watendaji wa sekta ya hifadhi ya jamii Afrika ili waweze kwa pamoja kujadili na kuazimia namna sekta hiyo ilivyokuwa na uwezo mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma nyingine za kijamii katika Bara la Afrika.

Jumuiya ya ASSA inaundwa na Mifuko ya Hifadhi Jamii kutoka nchi 15 za Bara la Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Sudan Kusini, Comoro, Cote d'ivoire, Gambia, Sierra Leone, Mali, Namibia na mwenyeji Tanzania. Kauli mbiu ya mkutano huo wa siku mbili ni "Sekta ya Hifadhi ya Jamii Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu kwa ajili ya masuala ya Kiuchumi na Kijamii katika Bara la Afrika"

MWISHO