News
NSSF YATUNUKIWA ISO 9001:2015, YAAHIDI HUDUMA BORA ZAIDI
*Yazindua Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026
Na Mwandishi Wetu
Kilimanjaro, Oktoba 5, 2026
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefikia hatua muhimu katika kuimarisha ubora wa huduma baada ya kutunukiwa Cheti cha ISO 9001:2015 cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kufuatia kukamilika kwa mchakato wa uhakiki na ithibati ya mfumo wake wa usimamizi wa ubora.
Hatua hiyo inaweka msingi muhimu kwa Mfuko kuendelea kuimarisha utendaji, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wanachama, waajiri na wadau wake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kitaifa wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Nurdin Babu, aliipongeza NSSF kwa kupata cheti hicho, akisema ni ishara ya juhudi zinazofanywa na Mfuko katika kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendelea kuimarika.
Mhe. Babu pia aligusia hatua ya Serikali ya kutoa msamaha wa tozo kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango, akiwataka kutumia fursa hiyo kurekebisha madeni yao na kuendelea kutimiza wajibu wa kulipa michango kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema katika jitihada za kuboresha huduma, Mfuko ulikamilisha mchakato wa kupata Cheti cha ISO 9001:2015 cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora hadi kufikia Juni 2026, hatua inayoonesha dhamira ya NSSF ya kuhakikisha huduma zake zinaendelea kutolewa kwa viwango bora.
“Cheti hiki kinaonesha dhamira ya Mfuko ya kuendeleza huduma bora na uwajibikaji. Hivyo, natumia nafasi hii kuwapongeza TBS kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kufanikisha upatikanaji wa cheti hicho, pamoja na watumishi wote wa NSSF,” alisema Bw. Mshomba.
Kwa mujibu wa Bw. Mshomba, Mfuko pia umepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo uandikishaji wa wanachama, ukusanyaji wa michango, uwekezaji, ulipaji wa mafao pamoja na matumizi ya TEHAMA.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yanaenda sambamba na ukuaji mkubwa wa Mfuko, ambapo thamani yake imeongezeka kutoka shilingi trilioni 9.8 Juni 2025, hadi shilingi trilioni 11.42 Juni 2026, sawa na ongezeko la asilimia 16.
“Mfuko umekua kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na kazi kubwa inayofanyika pamoja na ushirikiano kutoka kwa waajiri na wanachama. Hivyo, nampongeza Mhe. Rais kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, jambo ambalo limechangia ongezeko kubwa la waajiri,” alisema Bw. Mshomba.
Aidha, alisema NSSF imepiga hatua katika kuboresha utoaji wa mafao, ambapo wastani wa muda wa kushughulikia na kulipa mafao umepungua kutoka siku 63 mwaka 2021 hadi siku 19 katika mwaka wa fedha 2025/26.
Bw. Mshomba alisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yameendelea kurahisisha huduma kwa wanachama na waajiri, kwa kuwa sasa wanaweza kupata huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika ofisini, hatua inayolenga kupunguza usumbufu na kuongeza ufanisi wa huduma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari wa NSSF, Bw. Ibrahim Maftah, alisema kupata Cheti cha ISO 9001:2015 hakukuwa tukio la siku moja, bali ni matokeo ya juhudi za pamoja, mipango madhubuti, kujifunza, kujitathmini na kuboresha mifumo ya kazi kwa kipindi kirefu.
“Safari hii tuliianza kwa kupitia michakato yetu ya kazi, kuiboresha na kuhakikisha taratibu mbalimbali zinaendana na viwango vilivyowekwa. Tuliandaa nyaraka za mifumo ya ubora na kutoa mafunzo kuanzia ngazi ya Bodi ya Wadhamini hadi kwa watumishi wote. Baadaye ulifanyika ukaguzi na kubainika kuwa tumekidhi vigezo vyote vilivyowekwa, hatimaye tukatunukiwa cheti hicho,” alisema Bw. Maftah.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora, Mhandisi Abdallah Kileo, alisema cheti hicho ni ushahidi wa dhamira ya Bodi, Menejimenti na watumishi wa NSSF katika kuzingatia viwango vya kimataifa vya ubora.
Alisema cheti hicho kitasaidia kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kiwango kinachofanana katika ofisi za NSSF nchini, kupunguza urasimu na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma inayokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Ekwabi Mujungu, alisema ubora wa huduma unaanzia ndani ya taasisi, akiwataka watumishi kuvaa “viatu vya mwanachama na mteja” wanapotekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NSSF, Bw. Robert Kadege, alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 ni fursa ya kuwakumbuka na kuwashukuru wateja, kutambua mchango wa waajiri na watumishi, pamoja na kupata maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa.
Alisema maoni hayo ni muhimu katika kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha Mfuko unaendelea kukidhi na kuvuka matarajio ya wateja.
Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Audrey Claudius, alisema mkoa huo unaendelea kutoa huduma kupitia Ofisi ya Mkoa, Ofisi ya Wilaya ya Hai na vituo vya huduma vya Rombo, Same na TPC, huku ukitumia mifumo ya kidijitali kuongeza ufanisi.
Akifafanua mwelekeo wa NSSF, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Omary Mziya, alisema kaulimbiu ya “Huduma Bora kwa Vitendo” inapaswa kuonekana katika matokeo ya huduma, si maneno pekee.
Alisema NSSF itaendelea kuboresha michakato na mifumo, ikiwamo lango la huduma kwa waajiri na wanachama, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za michango, madai ya mafao na huduma nyingine.
Kwa hatua hiyo, NSSF inaendelea kujenga utamaduni wa ubora unaolenga kuhakikisha viwango vya huduma vinaendelea kuimarika, huku mahitaji na matarajio ya wanachama, waajiri na wadau yakiwekwa katika kiini cha utekelezaji wa majukumu ya Mfuko.
MWISHO

