News
JENGENI TIMU KAZI IMARA KUFIKIA MALENGO YA NSSF – MKURUGENZI WA UENDESHAJI NSSF

Na Mwandishi Wetu – Morogoro
Viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wametakiwa kuhakikisha wanajenga na kuimarisha timu kazi madhubuti katika maeneo yao ya kiutendaji ili kufanikisha malengo ya Mfuko kwa ufanisi zaidi, hususan katika ukusanyaji wa michango na ulipaji wa mafao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya, Mjinib Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha Mameneja wa Mikoa na Wakuu wa Vituo vya Wilaya. Kikao hicho kililenga kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na Mpango Kazi wa mwaka wa fedha 2025/26.
Bw. Mziya alisisitiza kuwa mafanikio ya Mfuko yanategemea kwa kiasi kikubwa katika utendaji kazi wa viongozi hao. Hivyo viongozi wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa ili yaweze kutoa matokeo chanya kwa wanachama na Taifa kwa ujumla.
“Performance ni namba. Wekezeni nguvu katika kuongeza tija ya utendaji kazi. Mfuko hauhitaji maneno mengi bali unahitaji takwimu halisi za utendaji kazi. Tukirudi kwenye maeneo yetu ya kazi, twende tukajenge namba za utendaji,” alisisitiza Bw. Mziya.
Aidha, aliwahimiza viongozi kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kuhakikisha malengo yote yaliyowekwa na Mfuko yanafikiwa bila kuiacha ofisi yoyote nyuma kiutendaji.
“Anzeni sasa kasi ya utendaji kazi. Ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha ujao, kila lengo liwe limefikiwa kama lilivyopangwa na uongozi wa Mfuko,” aliongeza Bw. Mziya
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa NSSF, Bw. Ekwabi Mujungu, aliwataka viongozi kuendelea kusimamia maadili ya wafanyakazi wao ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wanachama zinaakisi malengo na matarajio ya Mfuko.
Kikao kazi hicho kiliandaliwa na Kurugenzi ya Uendeshaji, ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa kutoka kurugenzi na vitengo vya Mfuko kama vile Ukaguzi wa ndani, Uhusiano na Elimu kwa Umma, Mambo ya Ndani,
TEHAMA, Mipango na Huduma kwa Wanachama.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za NSSF kuhakikisha kuwa viongozi wake katika ngazi zote wanakuwa na maono ya pamoja, uwajibikaji wa hali ya juu na mshikamano wa kiutendaji katika kufanikisha malengo ya Mfuko kwa ufanisi mkubwa.