emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA NSSF KWA USIMAMIZI BORA NA UPANUZI WA HUDUMA ZA HIFADHI YA JAMII KWA WOTE


Na. OWM (KAM), Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa usimamizi mzuri wa Mfuko na juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma za Hifadhi ya Jamii kwa wananchi, hatua inayochangia utekelezaji wa Dira ya 2050.

Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 15, 2026, jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, wakati kamati ilipopokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya NSSF katika kuwahudumia wanachama wa sekta binafsi, waajiri na waajiriwa pamoja na waliojiajiri.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya mfuko huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema NSSF inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za Hifadhi ya Jamii ili ziwanufaishe wananchi wengi zaidi, wakiwemo wale waliojiajiri.

Amesisitiza kuwa upanuzi wa huduma hizo ni muhimu katika kuimarisha ustawi wa wananchi na kuongeza uwezo wao wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii, sambamba na Nguzo ya Pili ya Dira ya 2050 inayolenga maendeleo ya watu na ustawi wa jamii.

Mhe. Sangu ameeleza kuwa katika kuimarisha wigo wa Hifadhi ya Jamii nchini, NSSF inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifumo ya Hifadhi ya Jamii , ikiwemo mpango wa Hifadhi Skimu ambao unalenga kuwafikia wananchi wasiokuwepo katika ajira rasmi ili nao wanufaike na huduma za Hifadhi ya Jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, amesema Mfuko huo umeweka mikakati ya kuongeza idadi ya wanachama kwa kuwafikia makundi mbalimbali ya wananchi, yakiwemo Mama na Baba lishe , maafisa usafirishaji madereva Boda boda , Bajaji, daladala na vyombo vingine vya usafirishaji, wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji wadogo wa madani , wasanii , wanamichezo na wafanyabiashara wadogo, ili waweze kupata ulinzi wa Hifadhi ya Jamii.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za NSSF kuhakikisha kuwa wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kujiwekea akiba na kujilinda dhidi ya changamoto zinazoweza kuathiri kipato na ustawi wao kila siku.

Kwa ujumla, pongezi za Kamati ya Bunge zinaonesha umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kupanua huduma zake ili kufikia makundi mengi zaidi ya wananchi, kwa lengo la kujenga jamii yenye usalama wa kipato na ustawi endelevu.