emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

MAMA JANET MAGUFULI APONGEZA HIFADHI SKIMU YA NSSF, AAHIDI KUIELIMISHA JAMII


Na MWANDISHI WETU,

Dar es Salaam. Mjane wa Rais wa Awamu ya Tano, Mama Janet Magufuli, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), ambapo amepongeza juhudi za Mfuko katika kuwaelimisha wananchi kuhusu Hifadhi Skimu, mpango unaolenga kuwajengea Watanzania msingi wa hifadhi ya kijamii kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Akizungumza baada ya kupata elimu kutoka kwa Meneja wa Sekta ya Wananchi Waliojiajiri wa NSSF, Bi. Rehema Chuma, Mama Janet alieleza kufurahishwa na hatua ya NSSF kuwawezesha Watanzania waliojiajiri kunufaika na mafao mbalimbali ya hifadhi ya jamii, yakiwemo ya matibabu, uzazi, ulemavu na pensheni ya uzee.

“Nashukuru NSSF kwa kuanzisha Hifadhi hii. Mimi naahidi kwenda kutoa elimu hii kwa vijana wangu ili wajue kuwa kuna kitu kizuri kitakachowasaidia kwa maisha ya sasa na baadaye,” alisema Mama Janet.

Kwa mujibu wa Bi. Rehema, Hifadhi Skimu inalenga makundi mbalimbali ya waliojiajiri kama vile wakulima, wavuvi, waendesha bodaboda, wachimbaji wadogo wa madini, mama na babalishe, waendesha bajaji, wasaidizi wa kazi za majumbani pamoja na wajasiriamali wengine.

“Mwanachama anaweza kuchagua kuchangia kuanzia shilingi 30,000 kwa ajili ya kujiwekea akiba na kunufaika na mafao yakiwemo ya matibabu yeye mwenyewe, au shilingi 52,200 ambapo atanufaika na mafao ya matibabu kwa mwanachama na wategemezi wake. Malipo yanaweza kufanyika kwa siku, wiki, mwezi au mwaka, kulingana na kipato,” alifafanua Bi. Rehema.

Aidha, Mama Janet alitaka kufahamu kwa undani kuhusu Hifadhi Skimu kama inawahusu wafanyakazi wa majumbani, ambapo alielezwa kuwa kundi hilo nalo linapaswa kujiandikisha ili kunufaika na mafao ya muda mfupi na mrefu yanayotolewa na Mfuko.

Bi. Rehema aliongeza kuwa huduma nyingi za NSSF sasa zinapatikana kidijitali kupitia simu ya mkononi, hivyo kuwawezesha wanachama kupata huduma popote walipo bila kufika ofisi za Mfuko.