emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​NSSF YAWEKA MIKAKATI YA KUONGEZA UFANISI NA HUDUMA BORA KWA WANACHAMA



Na MWANDISHI WETU,

Tanga. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema unatarajia kupata mafanikio makubwa zaidi kwa kuwa umewekewa vipaumbele vinavyolenga kupanua wigo wa wanachama, kuongeza mapato, kuboresha ulipaji wa mafao na kuimarisha huduma kwa wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA.

Aidha, umetoa rai kwa baadhi ya waajiri wa sekta binafsi nchini kuhakikisha wanawasilisha michango kwa wakati ili kuwezesha ulipaji wa mafao ya wanachama bila kuchelewa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 54 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi uliofanyika tarehe 8 Mei 2025 jijini Tanga, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema Mfuko unatarajia kuandikisha wanachama wapya 447,523 sawa na ongezeko la asilimia 15 huku mapato ya michango yakitarajiwa kufikia shilingi trilioni 2.99 kutoka trilioni 2.43 za mwaka unaomalizika.

“Tumejipanga kwa weledi na kasi kubwa. Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya hifadhi ya jamii bila ubaguzi. Hili linawezekana kwa kutumia TEHAMA, ubunifu na kuwafikia wananchi waliojiajiri”, amesema Bw. Mshomba.

Kwa mujibu wa Mshomba, mapato ya uwekezaji yanatarajiwa kupanda kwa asilimia 27 hadi kufikia bilioni 687.11 huku thamani ya vitega uchumi ikitarajiwa kufikia trilioni 10.17. Aidha, ulipaji wa mafao unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 21 na kufikia trilioni 1.13. “Katika mwaka wa fedha unaokuja thamani ya Mfuko inatarajiwa kuongezeka na kufikia trilioni 11.7 ifikapo mwezi Juni, 2026”, amesema Bw. Mshomba.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Bi. Mwamini Malemi, amesema Mfuko unaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma za hifadhi ya jamii kutokana na kasi ya uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, ongezeko la wanachama na uwekezaji wenye tija.

“Tunajivunia mafanikio haya. NSSF ni kielelezo cha taasisi inayobadilika kwa kasi, kwa manufaa ya wanachama”, amesema Bi. Mwalemi.

Awali, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Ekwabi Mujungu aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kuzingatia kwa makini maazimio watakayoyapitisha ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Mfuko.

Bi. Flora Ndutta, akitoa neno la shukrani amesema NSSF itaendelea kutoa huduma bora kwa kutumia TEHAMA, kuwafikia wananchi waliojiajiri na kwamba wataendelea kufanyakazi kwa bidii, kwa weledi na kwa kuzingatia maadili.

uchaguzi