News
NSSF YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KWA MAFANIKIO MAKUBWA
.jpeg)
Na MWANDISHI WETU,
Arusha. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeadhimisha kwa mafanikio makubwa ufunguzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka 2025 jijini Arusha, huku ukitangaza ongezeko kubwa la thamani ya Mfuko.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo katika Jengo la Mafao House, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema kuwa hadi kufikia Juni 30, 2025, thamani ya Mfuko imefikia shilingi trilioni 9.9 ikilinganishwa na trilioni 8.3 zilizorekodiwa Juni 30, 2024.
“Huu ni ushahidi wa wazi kwamba tunasonga mbele kwa kasi. Mafanikio haya yanakwenda sambamba na utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea. Tunajenga msingi imara wa uaminifu, uwazi na ushirikiano kati ya waajiri na wafanyakazi wa NSSF,” alisema Bw. Mshomba.
Alifafanua kuwa tangu kuingia madarakani kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwezi Machi 2021, thamani ya Mfuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.8 hadi trilioni 9.9, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100, akibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na usimamizi bora na imani kubwa ya wanachama.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanachama, waajiri, wastaafu na wachangiaji wa hiari, ambapo Mshomba alisisitiza kuwa Wiki ya Huduma kwa Wateja ni jukwaa muhimu la kuwashukuru wateja kwa mchango wao katika mafanikio ya Mfuko.
Katika kuunga mkono kampeni ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, NSSF ilitoa mitungi ya gesi kwa baadhi ya wanachama na wadau wake kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na kulinda mazingira.
“Tunataka kuhakikisha huduma za hifadhi ya jamii zinamfikia kila Mtanzania, wakiwemo wale waliojiajiri. Tunajitahidi kila siku kuongeza ubunifu na uwajibikaji ili wananchi wote wanufaike na hifadhi ya jamii,” alisema Bw. Mshomba.
@ofisi_ya_waziri_mkuu_kazi @owm_tz @onwm_tanzania @ridhiwani_kikwete @patrobasskatambi_ @msemajimkuuwaserikali @maelezonews
Edited · 1w
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wanachama wa NSSF, Bw. Robert Kadege, alisema NSSF inatumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kuwakumbusha wafanyakazi umuhimu wa kutoa huduma bora na kuwajulisha wanachama mageuzi ya kidijitali yanayoendelea.
“Sasa mwanachama anaweza kujihudumia popote alipo, na hata mstaafu anaweza kujihakiki bila kufika ofisini. Hii ni sehemu ya mageuzi ya kimfumo yanayoimarisha huduma kwa wateja wetu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa Mfuko unaendelea na kampeni ya “STAA WA MCHEZO” awamu ya pili “PAKA RANGI”, inayolenga kuongeza hamasa na elimu kwa wanachama hasa waliojiajiri, kutumia njia rahisi za kujiunga na kulipa michango yao kila mwezi, ili kupata mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF yakiwemo ya matibabu.
Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Ekwabi Mujungu, alisema NSSF imejipanga kuhakikisha kila mfanyakazi anatambua wajibu wake katika kutoa huduma bora kwa wateja, sambamba na kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa.
Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Bw. Josephat Komba, alibainisha kuwa Mfuko umeendelea kuwafuatilia waajiri wasiowasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati, ili kuhakikisha haki za wanachama zinalindwa ipasavyo.
Baadhi ya wanachama ambao ni wanufaika wa mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko, wameishukuru NSSF kwa kupata mafao mazuri pamoja na huduma bora zikiwemo za matibabu