emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YAENDELEA KUWAFIKIA WALIOJIAJIRI KUPITIA HIFADHI SKIMU


Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuwafikia wananchi waliojiajiri kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii kupitia Hifadhi Skimu, katika Jukwaa la wazi la fursa za biashara, uwekezaji na uanzishaji wa viwanda kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, lililofanyika wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoani Geita.

Kongamano hilo, lililopewa jina la “Fungua Fursa,” lilifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashimu Komba, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Alexander Mnyeti.

Elimu hiyo ilitolewa na Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele, kwa kushirikiana na Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Bi. Winniel Lusingu, ambapo walieleza manufaa ya kujiunga na NSSF kupitia Hifadhi Skimu, hususan kwa wananchi waliojiajiri.

Katika elimu hiyo, wananchi, wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini na maafisa usafirishaji (bodaboda), walihimizwa kutumia fursa ya Hifadhi Skimu kwa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye na kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko kwa mujibu wa sheria, yakiwemo mafao ya matibabu, uzazi, pensheni ya uzee, urithi na ulemavu.

Aidha, ilisisitizwa kuwa hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu katika ustawi wa wananchi, hivyo kuanza kuweka akiba mapema na kuendelea kuchangia kutawawezesha kujenga maisha yenye uhakika zaidi kwao na familia zao.

Ushiriki wa NSSF katika kutoa elimu hiyo unaendana na Dira 2050, inayolenga kujenga taifa lenye uchumi shindani na jumuishi, unaowawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kunufaika na matokeo ya maendeleo.

Kupitia Hifadhi Skimu, NSSF inaendelea kuwawezesha wananchi waliojiajiri kujenga ulinzi wa kijamii na kujiandaa kwa maisha ya sasa na ya baadaye.

Vilevile, utoaji wa elimu na uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Hifadhi Skimu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nane wa NSSF wa mwaka 2026/27–2030/31, unaolenga kupanua wigo wa hifadhi ya jamii na kuongeza idadi ya Watanzania wanaofikiwa na huduma za Mfuko, hususan wananchi waliojiajiri.

Katika hatua nyingine, NSSF ilitoa fulana maalumu zenye virejeshi mwanga vya usalama barabarani (reflector vests) kwa maafisa usafirishaji (bodaboda), ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono katika kuimarisha usalama wao wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Waendesha pikipiki hao ni miongoni mwa makundi yanayolengwa na Hifadhi Skimu, ambayo huwawezesha wananchi waliojiajiri kuweka akiba kwa ajili ya mafao ya uzeeni na baada ya kuchangia kwa miezi mitatu mfululizo, kunufaika na mafao ya matibabu pamoja na mafao mengine yanayotolewa kwa mujibu wa taratibu za Mpango huo.

Kupitia ushiriki wake katika matukio mbalimbali, NSSF inaendelea kusogeza elimu na huduma za hifadhi ya jamii karibu na wananchi, hususan makundi ya waliojiajiri, kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki katika hifadhi ya jamii pamoja na kujenga msingi imara wa ustawi wa wananchi na familia zao.

MWISHO