emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​NSSF YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA KWENYE SEKTA YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII NA HUDUMA ZA BIMA KATIKA MAONESHO YA KITAIFA YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA


* Yapata tuzo maalum

* Yatumia fursa ya maonesho kutoa elimu ya Hifadhi ya Jamii

Na Mwandishi Wetu

Geita, Oktoba 2, 2026 — Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeibuka mshindi wa kwanza katika Sekta ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Huduma za Bima katika Maonesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, na kutunukiwa tuzo maalum kwa kutambua ushiriki wake katika maonesho hayo.

Tuzo hiyo imetolewa Oktoba 2, 2026 na Mgeni Rasmi, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, Naibu Katibu Mkuu (Muungano), Ofisi ya Makamu wa Rais, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa taasisi, kampuni na vikundi mbalimbali vilivyoshiriki katika maonesho hayo.

Maonesho hayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Madini ni Utajiri – Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050”, yakilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali katika kujadili na kuonesha teknolojia na fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini.

Kupitia ushiriki wake, NSSF imeendelea kutumia jukwaa hilo kutoa elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi, hususan wafanyakazi wa sekta rasmi, wananchi waliojiajiri na wadau wa Sekta ya Madini.

Elimu hiyo imejikita katika huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko, ikiwemo mafao yanayotolewa, uandikishaji wa wanachama wapya, njia rahisi za kujiunga na huduma za NSSF kupitia simu za kiganjani, pamoja na fursa za uwekezaji katika miradi ya nyumba na viwanja.

Aidha, wananchi wamepatiwa elimu kuhusu huduma za kidijitali zinazotolewa na NSSF, ikiwemo NSSF Portal na NSSF App, pamoja na umuhimu wa kupambana na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma.

Pamoja na makundi mengine, wachimbaji wadogo wa madini, waendesha bodaboda na wajasiriamali wengine wameonesha mwitikio mkubwa kuhusu Hifadhi Skimu, mpango maalum unaowawezesha wananchi waliojiajiri kuweka akiba kwa ajili ya uzeeni, huku wakinufaika na mafao mbalimbali, ikiwemo matibabu baada ya kuchangia kwa miezi mitatu mfululizo bila kukatisha.

Mwitikio huo umewezesha baadhi ya wananchi kupata elimu ya kina kuhusu Hifadhi Skimu na kuchukua hatua ya kujiunga na kuanza kuchangia, hali inayoonesha umuhimu wa NSSF kuendelea kutumia maonesho na majukwaa mengine ya umma kuwafikia wananchi na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa Hifadhi ya Jamii.

MWISHO