News
NSSF Yahamasisha Waliojiajiri Kujiunga na Hifadhi Skimu Dodoma
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewahimiza wananchi waliojiajiri kujiunga na Hifadhi Skimu ili kujihakikishia usalama wa maisha yao ya sasa na baadaye kupitia mafao mbalimbali yanayotolewa.
Akizungumza Aprili 30, 2026 katika soko la Machinga jijini Dodoma wakati wa Kipindi cha Mkoleni kinachorushwa na C-FM Radio , Meneja wa NSSF Mkoa huo, Bw. Yahya Mudhihiri, alisema mpango huo unalenga kuwafikia makundi kama wakulima, wavuvi, bodaboda na wajasiriamali ambao awali hawakuwa na fursa ya hifadhi ya jamii.
Alieleza kuwa kiwango cha chini cha uchangiaji ni shilingi 30,000 kwa mwezi, huku shilingi 52,200 zikimwezesha mwanachama kujumuisha mwenza na watoto wasiozidi wanne. Mfumo wa uchangiaji umeboreshwa kuruhusu malipo kufanyika kwa siku, wiki, mwezi au msimu, pamoja na kutumia simu za mkononi kwa urahisi zaidi.
Bw. Mudhihiri alibainisha kuwa wanachama wa NSSF wakiwemo waliojiari hunufaika na mafao mbalimbali ya muda mrefu na mfupi yakiweno ya matibabu, uzazi na pensheni ya Uzee,hivyo kuwapa uhakika wa maisha hata wanapopoteza uwezo wa kufanya kazi.
Alisisitiza wananchi kuchangamkia fursa hiyo kama njia ya kujenga akiba na kujilinda dhidi ya changamoto za maisha ya baadaye.

