News
NSSF YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA MFUKO WA WCF

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Kazi (WCF), unatekelea kutekeleza majukumu yake vizuri ambapo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma kwa kuendelea kufanya vizuri katika Mfuko huo tangu kuanzishwa kwake
Mhe. Majaliwa alisema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya WCF yaliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Alisema kaulimbiu ya Mfuko huo “Miaka 10 ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi: Kazi Iendelee”, imebeba ujumbe unaoakisi mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka kumi tangu ulipoanzishwa Mfuko huo.
Mhe. Majaliwa alisema huduma za fidia kwa wafanyakazi sio suala la hiari bali ni suala la haki ya msingi kwa mfanyakazi ambayo inapaswa kulindwa, kuendelezwa na kusimamiwa kwa weledi na uwajibikaji wa hali ya juu.
Alisema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha maendeleo ya nchi, yanakwenda sambamba na ulinzi na haki na usawa wa wafanyakazi mahali pa kazi.
“Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wote ameendelea kutoa miongozo ya kuhakikisha kuwa Serikali itafanya maboresho ya maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla wake”, alisema Mhe. Majaliwa.
Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alikabidhi tuzo kwa waajiri na wadau waliotoa mchango mkubwa katika safari ya WCF, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba alikabidhiwa tuzo kwa mchango mkubwa alioutoa wakati alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa WCF.