emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

NSSF YAUNGA MKONO AJENDA YA NISHATI SAFI NA UHIFADHI WA MAZINGIRA KUELEKEA DIRA 2050


*Yakabidhi majiko janja, yapanda miti Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro

*Ni Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026

Na Mwandishi Wetu

Kilimanjaro, Oktoba 4, 2026

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeunga mkono ajenda ya Serikali ya matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira katika utekelezaji wa Dira 2050, kwa kukabidhi majiko banifu matatu na kupanda miti ya matunda na kivuli katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro.

Hatua hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kupunguza utegemezi wa kuni, kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha afya na kuchangia ustawi wa jamii.

Akizungumza katika zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, aliishukuru NSSF kwa kuunga mkono ajenda hiyo ya kitaifa, akisema matumizi ya nishati safi na upandaji miti ni hatua muhimu katika kulinda mazingira, afya za wananchi na kujenga maendeleo endelevu.

Alisema mazingira ni msingi wa shughuli mbalimbali za kiuchumi mkoani humo, zikiwemo kilimo, utalii na biashara, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kushiriki katika uhifadhi wake.

Mhe. Babu alihimiza uongozi wa shule na wanafunzi kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa hadi ikue na kutoa manufaa yaliyokusudiwa, yakiwemo matunda na kivuli.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kudhibiti ukataji holela wa miti, hususan katika maeneo ya vyanzo vya maji, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na urithi wa kizazi cha sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema zoezi hilo ni sehemu ya mwendelezo wa mchango wa Mfuko katika kuunga mkono ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira.

Alisema ajenda hiyo inaendana na Dira 2050, hususan katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kwamba NSSF imekuwa ikitekeleza shughuli za upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Dodoma na Mwanza.

Bw. Mshomba alisema matumizi ya majiko banifu yatasaidia kupunguza utegemezi wa kuni, moshi na uchafuzi wa mazingira, hivyo kulinda afya za wanafunzi na wapishi.

Alisema NSSF itaendelea kushirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa na majiko yaliyotolewa yanatumika ipasavyo, ili hatua hiyo ilete manufaa ya muda mrefu kwa shule na jamii.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Yusuf Nzowa, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, waliishukuru NSSF kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira, wakisema utoaji wa majiko banifu na upandaji miti ni hatua inayokwenda sambamba na ajenda ya Serikali na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya, na Meneja wa NSSF Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Audrey Claudius, walisema NSSF imeamua kutumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mazingira na matumizi ya nishati safi, kupitia utoaji wa majiko banifu na upandaji miti.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro, Mariana Msangi, aliishukuru NSSF kwa kuboresha mazingira ya shule kupitia upandaji wa miti na utoaji wa majiko banifu, akisema hatua hiyo itasaidia kujenga mazingira bora ya kujifunzia na kuwaelimisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi.

Hatua hiyo inaakisi dhamira ya NSSF ya kutekeleza wajibu wake kwa jamii kwa kuunga mkono vipaumbele vya Serikali, huku ikichangia kulinda mazingira, afya za jamii na kujenga mazingira salama na endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho, sambamba na utekelezaji wa Dira 2050. “Kwa mtazamo wangu, hii sasa ina mpangilio mzuri zaidi”. Alisema Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro.

MWISHO